Amnesty International: Mashia Nigeria wametoweka katika mazingira ya kutatanisha
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty international limetahadharisha kuhusu kutoweka mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia raia wa Nigeria na limeikosoa vikali serikali ya nchi hiyo kuhusiana na jambo hilo.
Amnesty International imekemea hali hiyo ya kutoweka Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria na imeitaka serikali ya Abuja kufanya uchunguzi kuhusu kutoweka kwa Mashia 600 nchini humo.
Taarifa ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu imetoa wito wa kuchukuliwa hatua na kuadhibiwa watu waliotenda jinai na uhalifu huo.
Taarifa ya Amnesty International inasema kuwa, Waislamu 350 wa madhehebu ya Shia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) waliuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la nchi hiyo katika kipindi cha tarehe 12 na 14 Disemba mwaka 2015 katika mji wa Zaria huko kaskazinini magharibi mwa Nigeria na wengine 600 hawajulikani waliko.
mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Nigeria pia akiwemo kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky wangali wanashikiliwa na vyombo vya usalama vya nchi hiyo bila ya kufikishwa mahakamani.