Waislamu Nigeria waendelea kulalamikia kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i33907-waislamu_nigeria_waendelea_kulalamikia_kushikiliwa_sheikh_ibrahim_zakzaky
Waislamu nchini Nigeria wameendelea kulalamikia hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuendelea kumshikilia kizuizini Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2017 09:27 UTC
  • Waislamu Nigeria waendelea kulalamikia kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky

Waislamu nchini Nigeria wameendelea kulalamikia hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuendelea kumshikilia kizuizini Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.

Hassan al-Banna mmoja wa wajumbe wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameziambia duru za habari kwamba, Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo wameendelea kulalamikia na kulaani hatua ya serikali ya nchi hiyo ya kuendelea kumshikilia Sheikh Ibrahim Zakzaky licha ya mahakama kutoa amri ya kuachiliwa huru mwanaharakati huyo wa Kiislamu.

Aidha amesema kuwa, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeishtaki katika Umoja wa Afrika AU serikali ya Rais Muhamadu Buhari kutokana na kukataa kumuachilia huru Sheikh Ibrahim Zakzaky.

Maandamano ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky

Itakumbukwa kuwa, Sheikh Ibrahim Zakzaky alitiwa nguvuni na jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 baada ya kuvamia makazi yake na kufanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu. Hata hivyo licha ya mahakama kutoa hukumu ya kutaka kuachiwa huru shakhsia huyo, bado vyombo vya usalama vya Nigeria vinaendelea kumshikilia katika korokoro isiyojulikana huku ripoti zikifichua kwamba hali yake ya kiafya ni mbaya.

Waislamu wa nchi hiyo wamekuwa wakifanya maandamano ya amani mara kwa mara ambapo wamekuwa wakisisitiza juu ya udharura wa serikali ya Nigeria kuheshimu sheria na hukumu ya mahakama ya nchi hiyo iliyotaka kuachiwa huru kiongozi wao.

Pamoja na hayo na licha ya kuweko miito mbalimbali ya asasi za kieneo na kimataifa za kutetea haki za binadamu  inayotaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, lakini serikali ya Rais Buhari hadi sasa imekataa kumuachilia huru mwanazuoni huyo wa Kiislamu.