Kamisheni ya Uchaguzi DRC yataka kusogezwa mbele uchaguzi
(last modified Sat, 19 Mar 2016 16:55:58 GMT )
Mar 19, 2016 16:55 UTC
  • Kamisheni ya Uchaguzi DRC yataka kusogezwa mbele uchaguzi

Kamisheni ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetoa wito wa kusogezwa mbele tarehe ya uchaguzi wa Rais na Bunge.

Corneille Nangaa, Mkuu wa Kamisheni ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametangaza kuwa, tume hiyo imewasilisha ombi la kubadilishwa tarehe ya uchaguzi katika Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo. Nangaa amesema kuwa, tume yake imeamua kuwasilisha ombi hilo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kuandaa na kufanya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo hapo Novemba mwaka huu. Amesema, Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (CENI) haina muda wa kutosha kutekeleza mpango kupitia upya orodha ya majina ya wa[piga kura.

Wapinzani wa serikali ya Kinshasa wanasema kuwa, takwa la kuakhirishwa uchaguzi ni njama za kutaka kumuongezea Rais Joseph Kabila muda wa kuendelea kubakia madarakani.

Kwa miezi kadhaa sasa, jamii ya kimataifa imekuwa ikisisitizia juu ya umuhimu wa kufanyika uchaguzi mkuu katika tarehe iliyopangwa huko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo huku waungaji mkono wa Rais Joseph Kabila wakitaka muda zaidi kwa ajili ya shughuli hiyo. Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Rais Joseph Kabila haruhusiwi kugombea tena katika uchaguzi ujao.

Wapinzani wamekuwa wakimtuhuma Rais Kabila kwamba, anafanya njama za kutaka kung'ang'ania madarakani.

Tags