Wakimbizi milioni moja Nigeria katika hatari ya kuambukizwa kipindupindu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34065-wakimbizi_milioni_moja_nigeria_katika_hatari_ya_kuambukizwa_kipindupindu
Zaidi ya wakimbizi milioni 1.4 nchini Nigeria ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram, hivi sasa wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa kipindipindu.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 08, 2017 02:53 UTC
  • Wakimbizi milioni moja Nigeria katika hatari ya kuambukizwa kipindupindu

Zaidi ya wakimbizi milioni 1.4 nchini Nigeria ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram, hivi sasa wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa kipindipindu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa wakimbizi hao wa ndani ya nchi sasa wanaishi katika kambi ambazo zimekumbwa na mripuko wa kipindupindu kutokana na ukosefu wa suhula za afya ya umma.

Ugonjwa huo umeripotiwa wiki iliyopita katika kambi ya wakimbizi ya Muna Garage huko Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno ambalo ni ngome ya magaidi wakufurishaji wa Boko Haram. Tayari watu 28 wameshapoteza maisha huku wengine 837 wakiambukizwa ugonjwa huo wakiwemo watoto 145 walio na umri wa chini ya miaka mitano.

Mashirika ya kutoa misaada yametahadahrisha kuwa, kuanza msimu wa mvua Nigeria kunaweza kueneza kipindupindu katika kambi za wakimbizi  ambazo hazina huduma za maji safi na maji taka.

Tokea Boko Haram ianzishe uasi wake nchini Nigeria mwaka 2009, watu 20 elfu wameshapoteza maisha. Aidha zaidi ya watu milioni mbili wamekuwa wakimbizi kutokana na ugaidi wa Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo ambalo lina ufahamu usio sahihi na potofu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likifanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.