Ombi la rais wa Nigeria la kujiepusha na kila aina ya ghasia
Kufuatia kuuawa idadi kadhaa ya raia wa Nigeria katika moja ya mapigano ya kikabila, Rais Muhamadu Buhari wa nchi hiyo, ametaka kuimarishwa usalama na utulivu nchini sambamba na kuwataka wananchi wajiepushe na vitendo vya utumiaji mabavu na ghasia.
Katika ujumbe wake Buhari ametaka kukomeshwa mauaji na kusisitiza kuwa, vyombo vya usalama tayari vimechukua hatua kwa ajili ya kuliokoa jimbo la Plateau kutokana na machafuko na mauaji yanayosababishwa na chuki za kikabila. Matamshi ya Rais Buhari yametolewa baada ya watu wenye silaha kufanya shambulizi dhidi ya kijiji kimoja katika jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria ambapo kwa akali watu 19 waliuawa na wengine watano kujeruhiwa. Nigeria ina makabila yapatayo 250 ambapo kila mwaka makumi ya raia hupoteza maisha katika mapigano ya kikabila yanayojiri katika maeneo tofauti ya nchi hiyo hususan maeneo ya katikati na kusini mwa nchi. Utumiwaji wa ardhi na vyanzo vya maji, unatajwa kuwa changamoto kubwa kati ya makabila tofauti nchini humo, jambo ambalo pia linachochea mapigano ya kikabila.
Mapigano kati ya wakulima na wafugaji juu ya utumiaji wa ardhi, kwa mara kadhaa yamesababisha maafa nchini humo. Aidha tofauti za kidini na kimadhehebu ni chanzo kingine cha kujiri mapigano na utumiaji mabavu, hususan katika miaka ya hivi karibuni. Inafaa kuashiria kuwa, sehemu kubwa ya jamii ya Nigeria inaundwa na Wakristo na Waislamu. Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni tofauti za kidini, zimekuwa zikichangia pia kuibuka mapigano ya kikabila kiasi kwamba siku chache zilizopita vijana kadhaa wa kabila la Arewa waliwataka watu wa kabila la Igbo ambao akthari yao ni Waislamu, kuondoka katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria. Katika uwanja huo Said Abubakr, mmoja wa wanachama waandamizi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria sambamba na kukosoa siasa za sasa nchini humo amelaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni ya vijana wa kabila la Arewa dhidi ya watu wa kabila la Igbo.
Akthari ya wataalamu wa kisiasa wanaelezea kuwa kukosekana usawa serikalini na udhaifu wa vyombo vya sheria vya serikali kuu katika kudhibiti hali ya mambo ni moja ya sababu za ongezeko la mashambulizi hayo. Kwa mujibu wa wataalamu hao, kukosekana usawa, ndiko kunakopelekea raia wa Nigeria kutekeleza mashambulizi ya ulipizaji kisasi. Ongezeko la mapigano ya kikabila nchini Nigeria linajiri katika hali ambayo kwa muda sasa taifa hilo linakabiliwa na mgogoro wa uwepo wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram ambapo mashambulizi ya kundi hilo yamevuruga usalama na amani katika maeneo mengi ya nchi hiyo. Katika hali hiyo kuendelea machafuko yoyote ya ndani kunazidisha changamoto kwa Rais Muhamadu Buhari na serikali yake, hasa kwa kuzingatia kuwa hadi sasa baadhi ya majimbo yamewasilisha mapendekezo ya kutaka kujitenga na serikali kuu. Kama walivyosema baadhi ya wachambuzi wa mambo, ongezeko la tofauti na vita vya kikaumu nchini Nigeria ni matokeo ya siasa za uingiliaji mambo ya ndani ya taifa hilo la magharibi mwa Afrika ambapo kujitenga kwa baadhi ya majimbo kutadhamini maslahi ya pande hizo za kigeni.
Matatizo ya kiuchumi ni suala lingine ambalo limepigilia msumari wa matatizo kwa serikali ya Abuja. Hii ni kwa kuwa, uchumi wa Nigeria umekumbwa na mdodoro tangu nusu ya mwanzo ya mwaka jana kutokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, suala ambalo limeyafanya maisha ya raia wa nchi hiyo kuwa magumu na hivyo kuongezeka malalamiko dhidi ya serikali. Kuhusiana na suala hilo Malte liewerscheidt mchafumbuzi wa masuala ya Kiafrika anasema: "Ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi nchini Nigeria, serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka za kivitendo." Mwisho wa kunukuu. Inaonekana kuwa katika hali ambayo mapambano dhidi ya ugaidi bado hayajazaa matunda, hivyo kuongezeka matatizo ya kiuchumi na kadhalika vita vya kikabila nchini, ni changamoto kubwa kwa serikali ya Rais Muhamadu Buhari.