Dola milioni 9.9 zahitajika kukabiliana na kipindupindu Borno Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34545-dola_milioni_9.9_zahitajika_kukabiliana_na_kipindupindu_borno_nigeria
Umoja wa Mataifa na washirika wake wametoa wito kwa wahisani wakihitaji msaada wa dola milioni 9.9 kukabiliana na mripuko wa kipindipindi uliozuka hivi karibuni katika Jimbo la Borno, kaskazini-mashariki mwa Nigeria.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 18, 2017 22:08 UTC
  • Dola milioni 9.9 zahitajika kukabiliana na kipindupindu Borno Nigeria

Umoja wa Mataifa na washirika wake wametoa wito kwa wahisani wakihitaji msaada wa dola milioni 9.9 kukabiliana na mripuko wa kipindipindi uliozuka hivi karibuni katika Jimbo la Borno, kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA,  jitihada  za kuzuia na kukabiliana na mlipuko huo zimeimarishwa ili kushughulikia mahitaji ya haraka  ya watu  wapatao milioni 3.7  ambao wako hatarini  kuambukizwa.

Licha ya juhudi kubwa za kuboresha usafi wa mazingira katika makambi na kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa mazoea  ya usafi,  matukio ya kwanza ya kipindupindu  yalitokea  katika Jimbo la Borno tarehe 16 Agosti. Hadi sasa, watu wapatao  44 tayari wamepoteza maisha kutokana na mlipuko huo, kati ya visa 2,300 vilivyothibitishwa.

Naye Mratibu wa OCHA Nigeria Lundberg  amesema  wanahitaji mbinu sahihi ya kukabiliana  na mlipuko huo ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu walioko kwenye maeneo yenye migogoro. Ameongeza kua mashirika ya kibinadamu yamekuwa yakifanya kazi  kwa ukaribu  sana na  wizara ya afya jimboni  Borno ili kuzuia kuzuka  kwa kipindupindu  katika maeneo mengi.

Jimbo la Borno ni ngome ya kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limekuwa likitekeleza hujuma za kigaidi kaskazini mwa Nigeria na kupelekea kuporomoka huduma za afya eneo hilo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram yaliyoanzia kaskazini mwa Nigeria na kusambaa hadi ndani ya ardhi za nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger yameshaua zaidi ya watu 20,000 katika eneo lote la Bonde la Ziwa Chad linalojumuisha nchi hizo nne, mbali na kuwafanya watu wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makaazi.