Wanawake wanaovaa Hijabu Nigeria wanasumbuliwa
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu Nigeria amekosoa namna wanawake Waislamu wanaovaa Hijabu nchini humo wanavyosumbuliwa.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake katika Kongamano la Kitaifa la Baraza Kuu la Masuala ya Kiislamu Nigeria, Alhaji Muhammad Sa’ad Abubakar III alisema Waislamu wanapaswa kupewa ruhusa ya kutekeleza misingi yao ya kidini kwa mujibu wa maamurisho ya Mwenyezi Mungu SWT na Sunna ya Mtume SAW.
Alhaji Abubakar aliongeza kuwa, uhuru wa kuabudu uko wazi katika katiba ya Nigeria na hivyo ni jambo linaloshangaza kuona Waislamu nchini humo wananyimwa haki zao na kubughudhiwa kwa sababu tu wanazingatia vazi la Hijabu. Kauli hiyo imekuja baada ya wakili mmoja Muislamu kunyimwa leseni ya kufika mahakamani kwa sababu ya kuvaa Hijabu.
Hivi karibuni wanafunzi Waislamu katika shule moja jimboni Gun kusini magharibi mwa nchi hiyo walilalamikia rasmi hatua ya shule yao kuwazuia kuvaa Hijabu.
Waislamu nchini Nigeria wamekuwa wakilalamikia sheria za baadhi ya majimbo ya nchi hiyo za kupiga marufuku vazi la hijabu katika shule binafsi hasa katika maeneo ambayo wakazi wake wengi ni Wakristo.

Ikumbukwe kuwa, mapema mwezi Februari mwaka huu, Mahakama ya Rufaa katika jimbo la Lagos nchini Nigeria ilitoa hukumu ya kubatilisha amri ya serikali ya jimbo hilo ya kupiga marufuku vazi la Hijabu kuvaliwa na wasichana Waislamu shuleni.
Aidha mapema mwaka huu muungano huo wa makundi ya wanawake wa Nigeria yanayozijumuisha taasisi kama vile za Al- Muminat, The Criterion, Mulism Society of Nigeria, MSSN, Federation of Muslim Women Association of Nigeria na nyingine kadhaa zimeitaka serikali kutoa adhabu kali kwa maafisa wake wanaowadhalilisha wanawake wanaovaa hijabu. Mratibu wa muungano huo Bi Hajia Mutiat Orolu-Balogun alisema katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hijabu kuwa, kuvaa vazi la stara la hijabu ni haki yao ya kikatiba ambayo inapaswa kulindwa na serikali kupitia sheria.