Msafara wa maafisa wa UN Nigeria washambuliwa, 4 wauawa
Maafisa wanne wa Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa WFP wameuawa baada ya msafara wao kuviziwa na kushambuliwa kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Taarifa ya WFP imesema kuwa, msafara huo ulishambuliwa na genge la watu waliokuwa wamejizatiti kwa silaha katika eneo la Ngala, yapata kilomita 35 kusini magharibi mwa jimbo la Borno.
Haijabainika iwapo waliotekeleza ukatili huo ni wanachama wa genge la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram au la.
Mwaka jana Umoja wa Mataifa ulisimamisha shughuli za kufikisha misaada ya kibinadamu katika eneo hilo la Borno, baada ya msafara mwingine wa wafanyakazi wake kushambuliwa na wanachama wa Boko Haram, ambapo watu kadhaa waliuawa.
Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram kuwakamata watu watano waliokuwa wakikimbia kutoka katika eneo la Damboa lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kuwaua kinyama.
Genge hilo la wakufurishaji lilizuka nchini Nigeria mwaka 2009 na hadi hivi sasa limeshasababisha zaidi ya watu 20 elfu kuuawa na wengine milioni 2 na laki sita kuwa wakimbizi huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.