Dec 28, 2017 16:34 UTC
  • Rais wa Uturuki: Quds ni mstari mwekundu kwa Ulimwengu wa Kiislamu

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kuuwa, Quds ni mstari mwekundu kwa Ulimwengu wa Kiislamu.

Rais Erdogan amesema hayo mjini Tunis Tunisia katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa pamoja na mwenyeji wake Rais Beji Caid Essebsi wa nchi hiyo ambapo sambamba na kubainisha kwamba, Ulimwengu wa Kiislamu unaitambua Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa Palestina amesema kwamba, uamuzi wa Marekani wa kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv na kuupeleka katika mji wa Beitul-Muuqaddas ni kinyume cha sheria.

Rais wa Uturuki amekosoa vikali pia muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kura ya veto ya Marekani kwa azimio lililowasilisha dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia akimkaribisha Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki

Rais Erdogan amesisitiza kuwa, ulimwengu ni mkubwa zaidi ya nchi tano zenye haki ya kura ya veto, lakini kwa nini nchi moja iwe na uwezo wa kuukwamisha mwenendo wa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa?

Recep Tayyip Erdogan amesema pia kuwa, Uturuki na Tunisia zitaendelea kuunga mkono vita dhidi ya ugaidi na kubainisha kwamba, Ankara inafanya hima ili kuhakikisha Tunis inakuwa na ustawi na uthabiti. Kwa upande wake Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia ameeleza azma ya nchi yake ya kuendeleza ushirikiano wa kibiashara na Uturuki. Tunisia ndicho kilichokuwa kituo cha mwisho cha safari ya kiduru ya Rais wa Uturuki barani Afrika, ambaye kabla ya hapo alizitembelea Sudan na Chad.

Tags