Kuongezeka majeshi ya nchi kubwa barani Afrika
Hatari ya kueneza zaidi ugaidi barani Afrika ndiyo kisingizio kinachotumiwa sasa na nchi kubwa hususan za Magharibi kwa ajili ya kuhalalisha kuwepo kwa majeshi ya nchi hizo barani Afrika na hilo linaonekana zaidi katika matamshi ya Rais Emanuel Macron wa Ufaransa aliyeiomba China kushirikiana na nchi za kundi la Sahil huko Afrika.
Matamshi hayo ya Macron yametolewa baada ya Waziri wa Ulinzi wa China, Chang Wanquan kusema katika mkutano wa kwanza wa ushirikiano wa kijeshi wa China, Afrika na nchi za Kiarabu uliofanyika tarehe 5 hadi 8 mwezi huu wa Januari huko Shanghai kwamba kumekuwepo ongezeko la mazoezi ya pamoja na ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo na kuanzisha timu za kitaalamu barani Afrika.
Japokuwa majeshi ya nchi mbalimbali za Magharibi na washirika wao yamekuwepo katika nchi za Afrika kwa kisingizio cha kuimarisha au kurejesha amani na kupambana na ugaidi, lakini uwepo wa majeshi hayo umeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kuongezeka tishio la ugaidi na mashambulizi yanayolenga baadhi ya nchi za Ulaya na vilevile kushindwa kundi la kigaidi la Daesh katika nchi za Iraq na Syria na uwezekano wa wanachama wake kukimbilia katika baadhi ya nchi za Kiafrika. Kwa mfano tu hivi karibuni maafisa wa Marekani walitangaza waziwazi kwamba, nchi hiyo imezidisha idadi ya wanajeshi wake barani Afrika. Seneta Lindsey Graham anasema: "makundi ya kigaidi yanaelekeza harakati zao barani Afrika na baada ya Mashariki ya Kati sasa Afrika imekuwa eneo la pili la operesheni za kijeshi za kikosi maalumu cha jeshi la Marekani."

Wakati huo huo Paris ndiyo iliyotoa pendekezo la kuanzishwa kikosi cha kundi la nchi tano za eneo la Sahel Afrika zikishirkiana na wanajeshi wa Ufaransa kwa ajili ya kupambana na ugaidi katika eneo hilo la kaskazini mwa Afika. Hii ni pamoja na kuwa China na Russia pia zimeanzisha harakati kubwa barani huo hususan katika nyanja za uchumi. Mwaka 2009 China iliipiku Marekani na kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa bara Afrika na sambamba na harakati hizo za kiuchumi, Beijing pia inaendelea kupanua ushirikiano na uhusiano wake wa kisiasa na kijeshi na nchi za bara hilo. Hivyo hivyo Russia ambayo imefunga mikataba mingi ya mauzo ya silaha kwa nchi za Afrika, kutoa mafunzo ya kijeshi sambamba na kupanua zaidi harakati zake za kiuchumi.

Afrika inahesabiwa kuwa soko lenye idadi kubwa ya jamii ya watu, ujari wa maliasili na maeneo mengi ya kistratijia. Hivyo nchi kubwa hususan za Magharibi mbali na kuwania utajiri na maliasi za nchi za bara hilo, zinafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba, zinazidisha uwepo wa majeshi yao katika maeneo mbalimbali ya bara hilo kwa kutumia visingizio mbalimbali au kupitia njia ya kukuza na kutia chumvi hatari kama ile ya ugaidi.