Makumi wapoteza maisha Nigeria kutokana na homa ya Lassa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41001-makumi_wapoteza_maisha_nigeria_kutokana_na_homa_ya_lassa
Wizara ya Afya ya Nigeria imetangaza kuwa makumi ya watu wamefariki dunia nchini humo kutokana na maambukizi ya homa ya Lassa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 01, 2018 01:07 UTC
  • Makumi wapoteza maisha Nigeria kutokana na homa ya Lassa

Wizara ya Afya ya Nigeria imetangaza kuwa makumi ya watu wamefariki dunia nchini humo kutokana na maambukizi ya homa ya Lassa.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya ya Nigeria imesema kuwa, kesi 193 za maambukizi ya homa ya Lassa zimeshuhudiwa katika majimbo 17 ya nchi hiyo kwenye kipindi cha miezi miwili iliyopita na kwamba watu 43 wamefariki dunia kutokana na homa hiyo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na homa hiyo ni sawa na asilimia 24 ya kesi zote zilizothibitisha za ugonjwa huo kote nchini Nigeria. 

Wakati huo huo Shirika la Afya dunian WHO limesema kuwa idadi mpya ya waathirika wa homa ya Lassa ambayo imetolewa na  kituo cha kudhibiti magonjwa cha Nigeria-NCDC- inaonyesha kuwa kati ya Januari mosi na Februari 25 mwaka 2018 visa 1,081 vya homa ya Lassa viliripotiwa na kwamba watu 90 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo. 

Wizara ya Afya ya Nigeria imesema kwa kawaida ugonjwa wa homa wa Lassa husambaa katika kipindi cha ukame lakini sasa unashuhudiwa katika vipindi na misimu yote ya mwaka.

Ugonjwa wa homa ya Lassa ulishuhudiwa kwa mara ya kwana nchini Nigeria maka 1969 katika mji wa Lasa na kwa sababu hiyo ulipewa jina la mji huo. Ugonjwa huo unashabihiana sana na ule wa Ebola. 

Nigeria ambayo ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika haina suhula za kutosha za tiba na majaribio ya homa ya Lassa yanafanyika katika maabara tatu tu kote nchini humo. 

Dalili za ugonjwa huo ni homa, mtu kujisikia mnyonge, baada ya siku chache mgonjwa huanza kuumwa na kichwa, kuwashwa na koo, kuumwa na kifua, kutapika, kuharisha, na kusokotwa na tumbo. Vilevile uso wa mgonjwa  unaweza kufura, kuumwa na mapafu na kutokwa damu mdomoni.

Homa hiyo hukaa mwilini kati ya siku 6 na 21.