Rais Mnangagwa ashangazwa na kusajiliwa vyama 112 vya siasa Zimbabwe
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ameeleza kushtushwa na ripoti zinazosema kuwa nchi hiyo imesajili makumi ya vyama vya siasa vitakavyochuana na chama tawala Zanu-PF katika uchaguzi mkuu ujao.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya NewsDay, Mnangagwa amesema karibuni hivi ataagiza uchugunguzi ufanyike kubaini uhalali wa kusajili kwa vyama 112 kufikia sasa nchini humo katika kipindi cha miezi michache iliyopita.
Kufikia Oktoba mwaka jana, Tume Taifa ya Uchaguzi Zimbabwe ZEC ilikuwa imesajili vyama 75 vya siasa, vilivyotangaza azma ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao, huku vingine vingi vikisajiliwa baada ya hapo.
Siku chache zilizopita, Rais Mnangagwa alisema Wazimbabwe watakuwa na fursa ya kumchagua kiongozi wao mwezi Julai mwaka huu, na wala sio mwezi Agosti kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali.
Kadhalika alisisitiza kuwa, uchaguzi huo wa Rais, Bunge na serikali za mitaa nchini Zimbabwe utafanyika katika mazingira huru na ya haki.