Mke wa Mugabe wa Zimbabwe achunguzwa kwa magendo ya vipusa
-
Grace Mugabe akiwa na mumewe, Robert Gabriel Mugabe
Serikali ya Zimbabwe imeanzisha uchunguzi dhidi ya mke wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe kwa tuhuma za kuhusika na magendo ya vipusa.
Uchunguzi huo umeanzishwa baada ya ufuatiliaji na upekuzi wa miezi mitatu uliofanywa na mpiga picha mashuhuri wa mbuga za wanyamapori raia wa Australia, Adrian Steirn.
Mpiga picha huyo wa Australia ameliambia shirika la habari la al-Jazeera kuwa, kuna mtandao mkubwa wa majangili ambao umekuwa ukiwaua ndovu na kung'oa pembe zao, na kisha kumuuzia Grace Mugabe kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Amesema ana picha za ushahidi zinazoonyesha kuwa baadhi ya ndovu hao waling'olewa pembe hizo wakiwa hai. Ifahamike kuwa, biashara ya vipusa ni halali nchini Zimbabwe iwapo utapewa kibali na serikali, lakini pembe hizo za ndovu au vifaru hazipaswi kuuzwa nje ya nchi.
Hivi karibuni, viongozi wa Afrika walimkosoa vikali Rais Donald Trump wa Marekani, kwa kuangalia upya sheria inayoiruhusu Washington kununua vipusa kutoka nchi za Afrika kama vile Botswana, Tanzania, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na Namibia.
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, bara la Afrika lilikuwa na ndovu milioni 13 mwaka 1979, lakini kushadidi magendo ya vipusa kumesababisha idadi hiyo kupungua hadi laki 4 hivi.