Polisi Nigeria waua mshiriki wa maandamano ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43206-polisi_nigeria_waua_mshiriki_wa_maandamano_ya_kutaka_sheikh_zakzaky_aachiliwe_huru
Mtu moja ameuawa baada ya polisi ya Nigeria kuwafyatulia risasi watu waliokuwa wakiandamana kwa amani wakitaka kiongozi wa harakati ya Kiislamu nchini humo, Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Apr 16, 2018 23:12 UTC
  • Polisi Nigeria waua mshiriki wa maandamano ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

Mtu moja ameuawa baada ya polisi ya Nigeria kuwafyatulia risasi watu waliokuwa wakiandamana kwa amani wakitaka kiongozi wa harakati ya Kiislamu nchini humo, Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.

Taarifa zinasema katika maandamano hayo yaliyofanyika jana Jumatatu katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, watu kadhaa walijeruhiwa baada ya kufyatuliwa risasi na polisi.

Kiongozi wa vijana katika Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Abdullahi Muhammad amesema walipoanza maandamano yao ya amani, polisi waliwafyatulia risasi na kuwarushia gesi ya kutoa machozi.

Amesema walishuhudia namna polisi walivyowachukua baadhi ya watu waliokuwa na majeraha ya risasi na kuwaweka ndani ya magari yao huku wakiwakalia. Ameelezea wasiwasi wake kuwa yamkini idadi ya waliofarikia ikawa kubwa.

Naye msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria Ibrahim Musa amesema polisi walitumia nguvu ziada dhidi ya watu waliokuwa wakiandamana kwa amani. Amesema takwa lao la kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe ni takwa la amani lakini polisi wamekuwa wakiendesha propaganda chafu dhidi ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Ameongeza kuwa Sheikh  Zakzaky daima ni mtu wa amani na kwamba nyuma yake lilikuwa kimbilio la watu wote waliodhulumiwa wakiwemo Wakristo. Waislamu wa Nigeria wamesisitiza kuwa wataendelea kuandamana kwa amani wakitaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru.

Maandamano ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashtaka.

Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo .