Tuhuma mpya za serikali ya Nigeria dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky
-
Sheikh Ibrahim Zakzaky akihojiwa na vyombo vya habari
Katika hali ambayo serikali ya Nigeria inaendelea kumshikilia kinyume cha sheria kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria na kukaidi hukumu ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo illiyoamrisha aachiliwe huru, sasa hivi serikali ya Abuja imezuka na tuhuma mpya dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna imetoa tuhuma mpya dhidi ya Sheikh Zakzaky kama vile kufanya mikutano kinyume cha sheria na kuvuruga utulivu, imedai kuwa wafuasi wa harakati hiyo walikuwa na silaha za hatari.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walijeruhiwa vibaya na kukamatwa katika shambulizi lililofanywa na jeshi la Nigeria tarehe 13 Disemba 2015 katika Husainia ya mji wa Zaria huko Kaduna, kaskazini mwa Nigeria. Mamia ya wafuasi wa harakati ya Kiislamu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky waliuliwa shahidi katika uvamizi huo wa jeshi la Nigeria. Ijapokuwa muda mfupi baadaye, Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe, lakini hadi hivi sasa jeshi na serikali ya nchi hiyo inaendelea kukaidi amri hiyo ya mahakama.
Hivi sasa imeshapita zaidi ya miaka miwili tangu alipokamatwa Sheikh Zakzaky, na licha ya mwanachuoni huyo kusumbuliwa na maradhi tofauti, lakini Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna imefumbia macho mambo yote hayo na kuzuka na tuhuma mpya dhidi ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria. Abdurrahman Yola, msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa tuhuma hizo mpya hazina msingi wowote na zimetolewa kama njia ya kuhalalisha kushikiliwa Sheikh Zakzaky na serikali ya Muhammadu Buhari, kinyume cha sheria.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, serikali ya Nigeria imelazimika kuzua tuhuma hizo mpya kutokana na kuongezeka mashinikizo ya Waislamu wanaolalamikia kuendelea kushikiliwa Sheikh Zakzaky kinyume cha sheria. Kwa muda sasa Waislamu wa Nigeria wanafanya mikusanyiko ya kupinga kuendelea kukiukwa amri ya mahakama ya kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu. Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Nigeria inaendelea kushikilia msimamo wake wa kiuadui dhidi ya Waislamu. Hivi karibuni polisi na vikosi vingine vya ullinzi vya Nigeria viliwashambulia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu na maandamano ya Waislamu wanaoshinikiza kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky na kujeruhi Waislamu kadhaa.
Abdulmumini Giwa, mmoja wa wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema: "Tutaendelea kupigania na kushinikiza kwa njia za amani kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky na kamwe hatutofanya fujo."
Ukandamizaji na vitendo vya chuki vya serikali ya Nigeria dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo vimeongezeka hivi sasa katika hali ambayo, weledi wengi wa mambo wanasema kuwa, chanzo hasa cha kuongezeka chuki hizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria ni chokochoko na ushawishi wa kisiasa na kiuadui wa Marekani, Israel na Saudi Arabia kwa serikali ya Rais Muhammadu Buhari. Kuendelea kufeli mtawalia siasa za utawala pandikizi wa Kizayuni katika eneo la Mashariki ya Kati kumeifanya kwa muda sasa Israel iamue kuelekeza nguvu zake katika pande nyingine za dunia likiwemo bara la Afrika. Saudi Arabia nayo imekuwa kwa muda mrefu ikitafuta kuwa na ushawishi barani Afrika. Misaada ya siri na ya dhahiri ya Saudia; kifedha na kijeshi; kwa nchi za bara hilo imekuwa ikitolewa kwa masharti ya nchi hizo kukubaliana na masharti ya Riyadh. Amma ushawishi wa Marekani huko Nigeria nao uko wazi. Weledi hao wanasema kuwa Marekani, Israel na Saudia zimeweza kujipenyeza sana ndani ya wanasiasa wa Nigeria na kueneza fikra zao za chuki dhidi ya Waislamu. Inavyoonekana ni kwamba tuhuma mpya zilizotolewa dhidi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky huko Nigeria ni sehemu ya kuendeleza vitendo vya chuki na mashinikizo dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo.