UN: Watoto laki 5 eneo la Ziwa Chad wanakodolewa macho na mauti
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45616-un_watoto_laki_5_eneo_la_ziwa_chad_wanakodolewa_macho_na_mauti
Umoja wa Mataifa umesema watoto karibu laki tano wanaoandamwa na utapiamlo wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na njaa katika nchi za eneo la Ziwa Chad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 09, 2018 03:42 UTC
  • UN: Watoto laki 5 eneo la Ziwa Chad wanakodolewa macho na mauti

Umoja wa Mataifa umesema watoto karibu laki tano wanaoandamwa na utapiamlo wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na njaa katika nchi za eneo la Ziwa Chad.

Hayo yamesemwa na Bintou Djibo, Mshirikishi wa Ofisi ya Uratibu ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Masuala ya Kibinaadamu (OCHA) nchini Niger katika kikao na waandishi wa habari mjini Geneva hapo jana na kuongeza kuwa, watoto nusu milioni katika nchi za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon huenda wakafa njaa iwapo nchi hizo hazitapokea misaada ya dharura haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa takwimu za UN, watu milioni tano katika nchi za eneo la Ziwa Chad hawana usalama wa chakula, ambapo watoto laki 4 na 90 elfu wanakabiliwa na utapiamlo wa kiwango cha juu, na wasipopata matibabu katika kipindi kifupi kijacho, watapoteza maisha.

Ramani inayoonesha nchi za eneo la Ziwa Chad

Mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram yamepelekea kuharibiwa ardhi za kilimo na kuwafanya wakazi wa maeneo mengi huko Ziwa Chad kulazimika kuyahama makazi yao.

Umaskini na njaa imekuwa sababu kwa wakazi wengi wa eneo la Ziwa Chad hususan vijana kujiunga na makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao katika eneo hilo kwa minajili ya kujidhaminia mahitaji yao muhimu.