Bunge la DRC kujadili sheria ya kuwalinda marais wa zamani
Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo litakutana katika kikao maalumu, kufuatia ombi la Rais Joseph Kabila, kwa lengo la kujadili sheria ya kuwapa kinga ya kisheria marais wa zamani wa nchi hiyo.
Tangazo hilo linatathminiwa kuwa ni ishara ya Rais Kabila kuazimia kuachia ngazi baad aya uchaguzi mkuu wa Disemba. Hayo yanajiri pamoja na kuwepo tetesi kuwa Kabila yamkini akawania tena urais pamoja na kuwa sheria inamzuia kufanya hivyo.
Waziri Mkuu wa DRC Bruno Tshibala amelimabia Shirika la Habari la Reuters kuwa Kabila hatagombea urais, hilo likiwa tamko la kwanza bayana la kiongozi wa ngazi za juu serikalini kuhusu kadhia hiyo.
Pamoja na kuwa Kabila bado hajatamka hadharani iwapo ataondoka madarakani, baadhi ya wafuasi wake wamekuwa wakijaribu kuwasilisha mapendekezo ya kisheria wanayosema yanamruhusu Kabila kuwania tena.
Spika wa Bunge Aubin Minaku amesema, 'kufuatia pendekezo la rais wa jamhuri, kikao kisicho cha kawaida kitafanyika bungeni. Bado haijabainika kikao hicho kitafanyika lini. Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya DRC, rais anayeondoka madarakani ana kinga ya kutoshtakiwa.
Kabila alichukua uongozi wa DRC mwaka 2001 baada ya baba yake kuuawa. Kwa mujibu wa katiba, alitakuwa kuondoka madarakani Disemba 2016 lakini uchaguzi wa atakayechukua nafasi yake umekuwa ukiahirishwa mara kwa mara. Hatua ya Kabila kuendelea kubakia madarakani imeibua mgogoro wa kisiasa nchini humo na kupelekea kuibuka maandamano makubwa ya wapinzani.