Eritrea yaondoa wanajeshi wake katika mpaka na Ethiopia
(last modified Thu, 19 Jul 2018 15:32:12 GMT )
Jul 19, 2018 15:32 UTC
  • Eritrea yaondoa wanajeshi wake katika mpaka na Ethiopia

Serikali ya Eritrea imewaondoa wanajeshi wake katika mpaka wake na Ethiopia uliokuwa ukilindwa vikali.

Shirika la habari lenye kuiunga mkono serikali ya Asmara la Eritrean Press limetangaza habari hiyo leo Alkhamisi na kuongeza kuwa, hatua hiyo ni ishara ya kuendelea kuimarika uhusiano wa Eritrea na Ethiopia.

Hata hivyo serikali ya Eritrea haijatoa maelezo yoyote kuhusu hatua hiyo kufikia sasa.

Hii ni katika hali ambayo, hapo jana ndege ya kwanza ya wasafiri kutoka Ethiopia ilitua katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara, kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20,  ikiwa ni ishara ya kuzidi kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili za Pembe ya Afrika ambazo zilihasimiana kwa miongo miwili kabla ya kurejesha uhusiano wiki za hivi karibuni.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki mjini Addis Ababa

Kadhalika siku ya Jumamosi, Eritrea ilifungua tena ubalozi wake nchini Ethiopia baada ya nchi hizo mbili jirani kumaliza uhasama wa miongoni miwili kuhusu mpaka.

Julai 9, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki walisaini makubaliano ya kukomesha uhasama na kuhuisha uhusiano wao wa kidiplomasia katika hafla iliyofanyika mjini Asmara. Eritrea ilijitenga na Ethiopia mwaka 1993  na kukata uhusiano wa pande mbili.

Tags