Mnangagwa: Wakulima wazungu wasiwe na hofu kuhusu ardhi zao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46936-mnangagwa_wakulima_wazungu_wasiwe_na_hofu_kuhusu_ardhi_zao
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amewafahamisha wakulima wazungu nchini humo kuwa zama za kuchukuliwa kwa nguvu ardhi zao zimemalizika huku akiwataka wafanye kazi pamoja na serikali yake.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Jul 22, 2018 07:23 UTC
  • Mnangagwa: Wakulima wazungu wasiwe na hofu kuhusu ardhi zao

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amewafahamisha wakulima wazungu nchini humo kuwa zama za kuchukuliwa kwa nguvu ardhi zao zimemalizika huku akiwataka wafanye kazi pamoja na serikali yake.

Mnangagwa ameyasema hayo katika mkutano wa kampeni kabla ya uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika Julai 30 ambapo mpinzani wake mkuu ni Nelson Chamisa wa chama cha upinzani cha MDC.

Mnangagwa alichukua madaraka mwezi Novemba baada ya jeshi kumuondoa madarakani rais wa muda mrefu wa nchi hiyo Robert Mugabe ambaye aliwahi kuongoza kampeni ya kuwapokonya mashamba wakulima wazungu na kuyagawa kwa wazalendo Waafrika.

Wakulima wazungu wa Zimbabwe wanakadriwa kuwa 30,000 na kwa kawaida hupigia kura vyama vya upinzani kutokana na uhusiano wao mbaya na chama tawala cha ZANU-PF cha Mnangagwa.

Akizungumza na wakulima 2000 wazungu Wazimbabwe Jumamosi katika mtaa wa Borrowdale katika mji mkuu, Harare, Mnangagwa amesema kuanzia sasa sheria itatumika katika kutatua mizozo ya ardhi. Amesema serikali yake inatilia maanani mchango wa kila mtu katika uchumi wa Zimbabwe huku akisema ni kinyume cha sheria kutazama wamiliki wa mashamba kwa rangi zao.

Shamba la zabibu nchini Zimbabwe

Amesema wakulima hawapaswi kubaguliwa kwa msingi wa rangi. Sekta ya kilimo Zimbabwe iliporomoka baada ya serikali ya Mugabe kuamua kuchukua kwa nguvu mashamba makubwa ya wazungu mwaka 2000. Aghalabu ya mashamba hayo yalinyakuliwa na wanasiasa vigogo, wanajeshi au machifu. Waliochukua udhibiti wa mashamba hayo hawakuwa na ujuzi wa kulima mashamba makubwa na hivyo sekta ya kilimo ikaporomoka.

Wakati huo huo, Kofi Anan, katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa anaongoza timu ya wasimamizi wa uchaguzi  nchini Zimbabwe na anasema ameridhika na kampeni zinavyoendelea.