Mnangagwa na Chamisa wasema wana matumaini ya kushinda uchaguzi wa Rais Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i47145-mnangagwa_na_chamisa_wasema_wana_matumaini_ya_kushinda_uchaguzi_wa_rais_zimbabwe
Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na mgombea wa chama cha MDC, Mchungaji Nelson Chamisa wamesema wote kuwa wana matumaini ya kushinda katika uchaguzi wa rais uliofanyika jana nchini humo.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Jul 31, 2018 15:58 UTC
  • Mnangagwa na Chamisa wasema wana matumaini ya kushinda uchaguzi wa Rais Zimbabwe

Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na mgombea wa chama cha MDC, Mchungaji Nelson Chamisa wamesema wote kuwa wana matumaini ya kushinda katika uchaguzi wa rais uliofanyika jana nchini humo.

Uchaguzi huo uliofanyika katika mazingira ya amani ni wa kwanza kufanyika nchini Zimbabwe baada ya uhuru wa nchi hiyo mwaka 1980 bila ya kumshirikisha kiongozi wa zamani aliyeondolewa madarakani, Robert Mugabe.p

Mnangagwa ambaye alichukua madaraka ya nchi Novemba mwaka jana baada ya jeshi la Zimbabwe kumlazimisha Mugabe kuondoka madarakani amesema kuna ripoti chanya kuhusu matokeo ya kura huku mpinzani wake mkubwa katika uchaguzi huo, Nelson Chamisa akisisitiza kuwa chama cha upinzani cha MDC kimefanya vizuri sana katika uchaguzi huo.

Wanadiplomasia wa nchi za Magharibi na makundi ya wasimamizi wa kikanda wanasema ushindani katika uchaguzi huo ulioshirikisha asimia 75 ya watu waliojiandikisha, ulikuwa mkali na kwamba kura za wapinzani hao wawili zinakaribia sana.

Kinara wa upinzani Nelson Chamis akipiga kura

Kamisheni ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC) imetangaza kuwa, hakukuripotiwa wizi au uchakachuaji wa kura.

Kwa upande wao waangalizi wa kundi la Zimbabwe Election Support Network (ZESN) wamesema kulikuwepo wasiwasi juu ya uhuru wa Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe (ZEC) kabla ya kufanyika zoezi hilo Jumatatu ya jana ingawa wamesisitiza kuwa kwa ujumla umefanyika kwa utaratibu mzuri ikilinganishwa na chaguzi za miaka iliyopita.

Matokeo kamili ya uchagui huo yatatangazwa Agosti 4.   

Zaidi ya Wazimbabwe milioni tano walijiandikisha kushiriki katika zoezi hilo la kumchagua rais mpya na wawakilishi wao bungeni.