Nigeria yawarahisishia raia wake kurejea nyumbani kwa hiari kutokea Libya
Serikali ya Nigeria kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) imeamua kuwarahishia njia za kurejea nyumbani kwa hiari raia wake waliokwama nchini Libya.
Kwa kushirikiana na shirika hilo, serikali ya Nigeria imekubali kutuma ndege za kuwarejesha nyumbani raia wake walioingia Libya kinyume cha sheria. Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa raia hao wa Nigeria wanaishi katika hali mbaya sana nchini Libya.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Lagos nchini Nigeria ndio utakaotumiwa kuwarejesha nyumbani raia wa nchi hiyo waliokwama nchini Libya.
Wimbi la wakimbizi haramu limeikumba Libya kutokana na kukosekana serikali yenye nguvu nchini humo na kutokana na kupakana kwake na bara Ulaya.
Kila mwaka maelfu ya wahajiri haramu wanahatarisha maisha yao kukimbilia barani Ulaya kwa kutumia bahari ya Mediterranean.
Wahajiri wengi haramu wanakimbilia Libya nchi ambayo yenyewe ilitumbukia kwenye machafuko mwaka 2011 baada ya Marekani na shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo katika kampeni za kuungasha utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.
Tangu wakati huo hadi hivi sasa nchi hiyo imeshindwa kuwa na utulivu wa angalau siku moja huku watu wanaokimbilia nchini humo wakipigwa mnada masokoni kama watumwa au kutumiwa vibaya na magenge ya kigaidi na ya magendo ya wanadamu.