Mahakama ya Katiba Zimbabwe yaanza kusikiliza kesi kuhusu uchaguzi wa rais
Mahakama ya Katiba nchini Zimbabwe inaanza kusikiliza leo, kesi ya chama kikuu cha upinzani MDC kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi rais Emmerson Mnangangwa.
Nelson Chamisa alikwenda Mahakamani baada ya kudai kuibiwa kura wakati wa uchaguzi mkuu mwisho wa mwezi Julai.
Nacho chama cha Rais Mnaganagwa Zanu-PF kimefika mahakamani kutaka kesi hiyo kutupiliwa mbali.
Upinzani nchini humo unasema Tume ya Uchaguzi ilimsaidia Mnangangwa kupata ushindi, na kudai kuwa kura za mgombea wake Nelson Chamisa ziliibiwa.
Wakili wa upinzani Thabani Mpofu, amesema tayari upinzani umeandaa ushahidi wa kutosha kuonesha namna kura zilivyoibiwa, na uko tayari kupambana na Tume ya Uchaguzi katika Mahakama hiyo ya katiba.
Mahakama ya Katiba ya Zimbabwe inatarajiwa kutoa uamuzi mmoja kati ya maamuzi matatu, ambayo ni kutupilia mbali kesi hiyo, kubatilisha ushindi wa Mnangagwa na kumtangaza Nelson Chamisa kuwa mshindi wa uchaguzi wa Julai 30 au kuitisha uchaguzi mwingine.
Hafla ya kuapishwa Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ambaye alishinda katika uchaguzi wa Julai 30 ambayo ilipangwa kufanyika Agosti 12, ilibidi iakhirishwe baada ya chama cha upinzani cha MDC cha Nelson Chamisa kuwasilisha kesi mahakamani kikipinga matokeo ya uchaguzi huo.

Uchaguzi wa kwanza wa Rais baada ya miaka 37 ya utawala wa Robert Mugabe ulifanyika nchini Zimbabwe tarehe 30 ya mwezi uliopita wa Julai.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, Emmerson Mnangagwa wa chama tawala cha ZANU-PF alishinda kwa kupata asilimia 50.8 ya kura huku mgombea wa chama cha MDC, Nelson Chamisa akipata asilimia 44.3 ya kura.