Mbivu mbichi kujulikana leo Zimbabwe kuhusu ushindi wa Rais Emmerson Mnangagwa
Raia wa Zimbabwe wana shauku kubwa ya kujua hukumu inayotazamiwa kutolewa na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo kuhusu kesi iliyowasilisha na kiongozi wa upinzani, Nelson Chamisa kupinga ushindi wa Rais Emmersom Mnangagwa katika uchaguzi uliofanyika Julai 30 mwaka huu.
Jaji Mkuu Luke Malaba anayeongoza jopo la majaji tisa ambao walikuwa wakisikiliza kesi hiyo, amenukuliwa akisema kuwa, uamuzi huo utatolewa majira ya saa nane mchana kwa majira ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika. Kufuatia hali hiyo, polisi wameonekana wakiimarisha usalama katika mitaa ya na njia za mji wa Harare na maeneo ya karibu na mji huo, sambamba na kufungwa badhi ya barabara za kuingia na kutoka miji hiyo. Baadhi ya duru zimetahadharisha juu ya uwezekano wa kutokea ghasia iwapo upande mmoja hautaridhishwa na uamuzi unaosubiriwa na mahakama ya katiba katika kesi hiyo. Chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) kinadai kuwa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi (ZEC) yaligubikwa na dosari nyingi, na hivyo kupendekeza kurudiwa upya uchaguzi wa raia au kutangazwa kuwa Rais wa Zimbabwe mgombea wake, Bwana Nelson Chamisa.
Wakili wa wakili wa chama cha MDC, Thabani Mpofu amewambia waandishi wa habari kwamba, karibu vituo 16 vya kupigia kura viliasajili matokeo sawa kwa wagombea wawili 'Chamisa na Mnangagwa' suala ambalo ni vigumu kutokea katika hali ya kawaida. “Udanganyifu mwingi ulitokea nah ii ndio maana Mnangagwa alipata ushindi mwembamba ili kumuepusha na hali ambayo ingepelekea uchaguzi urudiwe. Sharti matokeo hayo yafutuliwe mbali kwani ZEC ilishirikiana na chama cha ZANU-PF kumpokonya Bw Chamisa ushindi.” Amesema Mpofu. Kwa upande wake, wakili wa Rais Mnangagwa Thembinkosi Magwaliba, amepuuzilia mbali madai hayo akisema upinzani hauna ushahidi wowote kwamba uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu. “Kesi hii haina maana. Upinzani hauna ushahid wowote wa maana na bila shaka majaji watathibitisha ushindi wa ZANU-PF.” Amesema Magwaliba.