Aug 29, 2018 07:47 UTC
  • Riek Machar akubali kusaini makubaliano ya mwisho ya amani ya Sudan Kusini

Kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini amekubali kutia saini makubaliano ya mwisho ya mkataba wa amani na serikali ya Juba ambayo yatamaliza mgogoro wa muda mrefu wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.

Riek Machar ametangaza hatua yake hiyo masaa machache tu baada ya kutangaza kukataa kusaini mkataba huo wa amani na hasimu wake wa kisiasa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini.

Uamuzi wa Riek Machar wa kukubali kutia saini makubaliano ya amani ya Sudan Kusini umetangazwa na Dirdiri Mohamed Ahmed Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan ambaye ameeleza kwamba, makubaliano hayo ya amani sasa yatatiwa saini kesho Alkhamisi Agosti 30.

Mwezi uliopita Machar na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini walitia saini makubaliano ya kusitisha vita na kugawana madaraka. Makubaliano hayo yanayosimamiwa na Sudan yangali yanakabiliwa na changamoto kadhaa kuhusu namna ya utekelezaji wa baadhi ya vipengee vyake.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Mvutano wa kisiasa nchini Sudan Kusini uliibuka mwaka 2013 baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar kwamba anataka kumpindua. 

Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuyakimbia makazi na hata nchi yao huko Sudan Kusini kutokana na vita vya ndani baina ya jeshi la serikali ya Juba na kundi la waasi linaloongozwa na Riek Machar.

Asasi mbalimbali zimekuwa zikitahadharisha kuhusu kutokea maafa ya kibinadamu katika nchi hiyo.

Tags