Waafrika Kusini waandamana kupinga ukosefu wa amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i48522-waafrika_kusini_waandamana_kupinga_ukosefu_wa_amani
Maandamano yaliyofanywa na wakazi wa jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini kulalamikia hali mbaya ya ukosefu wa usalama yamegeuka na kuwa ghasia na machafuko makubwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 02, 2018 03:12 UTC
  • Waafrika Kusini waandamana kupinga ukosefu wa amani

Maandamano yaliyofanywa na wakazi wa jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini kulalamikia hali mbaya ya ukosefu wa usalama yamegeuka na kuwa ghasia na machafuko makubwa.

Ripoti zinasema kuwa, polisi wa mji wa Johannesburg wamekabiliana na waandamanaji hao kwa kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi za plastiki. 

Wakazi wa mji huo wamefanya maandamano baada ya mauaji ya mwanamke mmoja aliyeuawa Jumapili iliyopita kwa kupigwa risasi na magenge ya mafia na wafanya magendo ya dawa za kulevya.

Waandamanaji hao wameitaka serikali ya Afrika Kusini kuwajibika na kuimarisha usalama nchini humo. Baadhi ya waandamanaji hao wamesema kuwa, polisi ya Afrika Kusini inayalinda na kuyakingia kifua magenge yanayofanya biashara ya dawa za kulevya. Polisi inakanusha madai hayo. 

Ripoti zinasema kila siku watu wasiopungua 57 huuawa na makundi ya mafia na magenge ya biashara haramu ya dawa za kulevya nchini Afrika Kusini na kwamba serikali ya nchi hiyo haina mipango ya kupambana ipasavyo na makundi hayo.