Mahasimu wa Libya kuzungumzia uchaguzi katika kikao cha Italia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i49444-mahasimu_wa_libya_kuzungumzia_uchaguzi_katika_kikao_cha_italia
Makundi hasimu ya kisiasa ya Libya yanatazamiwa kukutana kesho Jumatatu katika mkutano wa kujadili masuala ya uchaguzi, utakaofanyika katika mji wa Palermo nchini Italia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 11, 2018 10:43 UTC
  • Mahasimu wa Libya kuzungumzia uchaguzi katika kikao cha Italia

Makundi hasimu ya kisiasa ya Libya yanatazamiwa kukutana kesho Jumatatu katika mkutano wa kujadili masuala ya uchaguzi, utakaofanyika katika mji wa Palermo nchini Italia.

Mkutano huo unafanyika siku chache baada ya Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salame, kuwasilisha mikakati mipya ya kufanyika Kongamano la Kitaifa na uchaguzi mkuu mapema mwaka ujao 2019.

Mbali na viongozi wa serikali hasimu za Tobruk na Tripoli, mkutano wa kesho utahudhuriwa pia na wajumbe wa Umoja wa Mataifa, Russia, Ufaransa na Marekani, kwa uenyeji wa Giuseppe Conte, Waziri Mkuu wa Italia.

Makundi ya wapiganaji Libya

Siku ya Alkhamisi, Salame aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, wananchi wa Libya wamechoshwa na uingiliaji wa kijeshi na mivutano ya kisiasa isiyokuwa na tija, na wanataka mustakabali mpya.

Tangu mwaka 2011 hadi sasa, Libya haijawahi kuwa na utulivu baada ya Marekani na NATO kuivamia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Hivi sasa kuna makundi ya kila namna yenye silaha nchini humo ambapo kila moja linapigania kuwa na nafasi kubwa zaidi.