UN yalaani kukandamizwa wapinzani Kongo DR kuelekea uchaguzi mkuu
Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali ukandamizaji, mbinyo na unyanyasaji unaofanywa na maafisa usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo dhidi ya wapinzani, siku chache kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.
Katika taarifa yake leo Ijumaa, Michelle Bachelet, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema, "Nina wasiwasi mkubwa kuhusu ripoti za utumiaji nguvu kupita kiasi, yakiwemo matumizi ya risasi hai dhidi ya mikusanyiko ya wapinzani. Misingi ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki inapasa kulindwa na vyombo vya dola, na serikali ya Kinshasa haina budi kuhakikisha kuwa inalinda haki na uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani."
Hapo jana, mfuasi wa Felix Tshisekedi, mmoja wa wagombea wa kiti cha urais kupitia chama cha upinzani cha Democracy and Social Progress (UDPS) aliuawa kwa kupigwa risasi na maafisa usalama katika eneo la Kasai.
Mauaji hayo yalifanyika siku moja baada ya watu wawili, wafuasi wa mgombea wa upinzani Martin Fayulu kuuawa kwa kufyatuliwa risasi na maafisa usalama huko Lubumbashi, mji wa pili kwa ukubwa nchini DRC. Polisi ya Kongo ilitumia risasi hai na mabomu ya gesi ya kutoa machozi kutawanya mkusanyiko wa wafuasi wa Martin Fayulu mjini hapo.
Taharuki imetanda nchini humo baada ya kushuhudiwa ghasia katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, ikiwa ni chini ya siku kumi kabla ya kufanyika uchaguzi huo wa Disemba 23.
Kushtadi ghasia hizo kumezidisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kukaririwa machafuko kama yale yaliyoshuhudiwa katika chaguzi za mwaka 2006 na 2011 nchini humo.