Polisi ya Afrika kusini yatoa waranti wa kukamatwa mke wa Mugabe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50284-polisi_ya_afrika_kusini_yatoa_waranti_wa_kukamatwa_mke_wa_mugabe
Polisi ya Afrika Kusini imetoa kibali cha kutiwa nguvuni mke wa rais wa zamani wa Zimbabwe, Grace Mugabe kwa tuhuma za kumshambulia na kumpiga mwanamitindo Gabriella Engels mjini Johannesburg mwaka uliopita.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Dec 19, 2018 15:21 UTC
  • Polisi ya Afrika kusini yatoa waranti wa kukamatwa mke wa Mugabe

Polisi ya Afrika Kusini imetoa kibali cha kutiwa nguvuni mke wa rais wa zamani wa Zimbabwe, Grace Mugabe kwa tuhuma za kumshambulia na kumpiga mwanamitindo Gabriella Engels mjini Johannesburg mwaka uliopita.

Mwanamitindo wa Afrika Kusini Gabriella Engels amemtuhumu Grace Mugabe kuwa alimshambulia na kumcharaza kwa waya wa umeme mwezi Agosti mwaka jana na kumsababishia majeraha katika paji la uso na nyuma ya kichwa.

Bi Grace alimtandika baada ya kumkuta msichana huyo akiwa pamoja na wana wawili wa kiume wa Mugabe wanaoishi Afrika ya Kusini.

Baada ya kesi hiyo kufikishwa mahakamani, serikali ya Afrika Kusini ilimpa mke wa Robert Mugabe, Grace kinga ya kidiplomasia. Hata hivyo kinga hiyo imetenguliwa na mahakama ya Afrika Kusini baada ya kusikiliza rufaa ya mwanamitindo Gabriella Engels.

Msemaji wa Polisi ya Afrika Kusini, Vishnu Naidoo amethibitisha kuwa mahakama imetoa waranti wa kutiwa mbaroni Bi Grace Mugabe na kwamba polisi ya nchi hiyo imeomba msaada wa Polisi ya Kimataifa (Interpol) kwa ajili ya kumtia nguvuni mtuhumiwa.

Mkuu wa kundi la AfriForum linalosimamia kesi hiyo, Kallie Kriel amesema uamuzi huo unatoa ujumbe kwamba hakuna mtu anayepaswa kuwa juu ya sharia hata kama atakuwa mke wa rais.