Katibu Mkuu wa UN ataka uchaguzi huru na wa haki Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50494-katibu_mkuu_wa_un_ataka_uchaguzi_huru_na_wa_haki_kongo_dr
Huku wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliotimiza masharti ya kupiga kura wakitazamiwa kuelekea katika masanduku ya kupigia kura kumchangua kiongozi atakayerithi mikoba ya Rais Joseph Kabila Jumapili ya kesho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa pande zote husika za kisiasa kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa uhuru na amani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 29, 2018 04:45 UTC
  • Katibu Mkuu wa UN ataka uchaguzi huru na wa haki Kongo DR

Huku wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliotimiza masharti ya kupiga kura wakitazamiwa kuelekea katika masanduku ya kupigia kura kumchangua kiongozi atakayerithi mikoba ya Rais Joseph Kabila Jumapili ya kesho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mwito kwa pande zote husika za kisiasa kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa uhuru na amani.

Antonio Guterres alitoa mwito huo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, "vyombo vya dola, viongozi wa kisiasa, maafisa wa uchaguzi na asasi za kiraia zinapaswa kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha kuwa kunakuweko na mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na wa haki, na kwa amani."

Guterres amewataka Wakongamani kutumia fursa hiyo ya uchaguzi aliyoitaja kuwa ya kihistoria, kuzipa nguvu taasisi za kidemokrasia nchini humo.

Tayari taasisi muhimu za ndani na nje ya nchi zimeelezea wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa kutokea machafuko wakati na baada ya zoezi hilo.

Wagombea wakuu wa urais nchini DRC

Hata hivyo taarifa ya Umoja wa Mataifa imewataka wadau wote kutekeleza wajibu wao na kujiepusha na kauli au vitendo vinavyoweza kuchochea ghasia ili kuhakikisha kuwa zoezi hilo la kidemokrasia linafanyika kwa amani.

Mbali na kuhitimisha uongozi wa Kabila ambaye yuko madarakani tokea mwaka 2001, wapiga kura pia watawachagua wabunge na wawakilishi wa mabunge ya mikoa.