Miungano ya wafanyakazi Zimbabwe yakataa nyongeza ya asilimia 10 ya mshahara
Watumishi wa umma nchini Zimbabwe kupitia miungano na vyama vya kutetea maslahi yao wamekataa nyongeza ya asilimia 10 ya mshahara iliyotangazwa na serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa jana Alkhamisi.
Wafanyakazi hao wa umma wamesema hawakubaliana na nyongeza hiyo iliyotangazwa na serikali, huku wakisisitiza kuwa wanataka kulipwa mishahara yao kwa kutumia sarafu ya dola ya Marekani.
Richard Gundane, Rais wa Chama cha Taifa cha Walimu ambaye alishiriki mkutano huo wa jana amesema "Wafanyakazi walitazamia kuwa mazungumzo kati yao na serikali yangejikita katika kutathmini uhalisia wa mambo, na nyongeza hiyo ambayo serikali inataka ianze kutekelezwa Aprili Mosi ingeanza kutekelezwa mara moja na ingezingatia mfumuko wa bei za bidhaa uliopo hivi sasa na gharama za juu za maisha."
Tangu Jumanne iliyopita, walimu nchini Zimbabwe wanafanya mgomo huku Rais wa nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa akiendelea kukabiliwa na mashinikizo ili kuipatia ufumbuzi hali ya kiuchumi inayolegalega sasa nchini humo.
Naye Thomas Muzondo, Rais wa Baraza la Apex ambalo ni mwavuli wa vyama 16 vya wafanyakazi wa umma amesema mkutano mwingine kati ya vyama hivyo vya watumishi wa umma na serikali unatazamiwa kufanyika wiki ijayo, na anatumai kuwa matarajio yao yataafikiwa.
Uhaba wa fedha umeyumbisha mfumo wa fedha wa Zimbabwe na kuzidisha uwezekano wa kuibuka ghasia. Kulegalega huko kwa hali ya uchumi Zimbabwe kunarudisha nyuma juhudi za Rais Mnangagwa za kuwavutia wawekezaji wa nje ambao waliwekwa kando wakati wa utawala wa Rais Robert Mugabe.
Serikali ya Zimbabwe imetangaza nyongeza hiyo ya asilimia 10, baada ya madaktari kukubali kusitisha mgomo wao wa siku 40 wa kushinikiza nyongeza ya mishahara na kuimarishwa mazingira ya kazi.