UN: Watu karibu 900 wameuawa katika mapigano ya kikabila DRC
Umoja wa Mataifa umesema watu zaidi ya 890 wameuawa katika ghasia za kikabila zilizotokea huko kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi uliopita wa Disemba 2018.
Hayo yalisema jana Jumatano na Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ambaye alisisitiza udharura wa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria wahusika wa jinai hiyo.
Idadi hiyo ya UN ni mara mbili zaidi ya idadi iliyotolewa Jumatatu iliyopita na asasi za kijamii na viongozi wa kidini nchini Kongo DR, waliosema kuwa waliouawa katika ghasia hizo za kikabila ni watu 400.
Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani amesema mapigano hayo ya kikabila katika mji wa Yumbi, magharibi mwa nchi yalisababisha pia wakazi 16,000 kati ya 18,000 waukimbie mji huo na kwenda katika maeneo mengine, huku baadhi yao wakikimbilia katika nchi jirani.
Kwa mujibu wa Gentiny Ngobila, Gavana wa mkoa wa Mai-Ndombe, watu 45 waliuawa na wengine 60 walijeruhiwa katika mapigano hayo ya kikabila yaliyotokea kati ya Disemba 15 na 16 magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo CENI ilitangaza kuakhirisha uchaguzi wa Disemba 30 mwaka jana katika mji huo wa Yumbi, baada ya watu zaidi ya 100 kuuawa katika machafuko ya kikabila; na sasa zoezi hilo linatazamiwa kufanyika mwezi Machi mwaka huu.