Sudan Kusini yapokewa rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
(last modified Sat, 16 Apr 2016 07:28:01 GMT )
Apr 16, 2016 07:28 UTC
  • Sudan Kusini yapokewa rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki

Ni rasmi sasa Sudan Kusini ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC. Hii ni baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kusaini mkataba unaorasimisha nchi hiyo kujiunga na EAC katika mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Dar es Salaam.

Rais Kiir amesaini mkataba huo mbele ya mwenyeji wake Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni mwenyekiti wa jumuiya hiyo ya kikanda.

Mwezi uliopita wa Machi, viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki waliidhinisha kwa kauli moja Sudan Kusini kujiunga na EAC. Uamuzi huo ulichukuliwa na viongozi wa EAC kwenye mkutano uliofanyika mjini Arusha, Tanzania mnamo Machi 2. Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ilisema viongozi wameridhia Sudan Kusini kuwa mwanachama wa 6 wa EAC baada ya kutimiza masharti yote yanayohitajika kwa mwanachama mpya. Sudan Kusini iliomba kujiunga na EAC punde baada ya kujitangazia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011, lakini mchakato wa kuiidhinisha nchi hiyo umekuwa ukisuasua kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni udhaifu kwenye taasisi muhimu za nchi hiyo pamoja na hali mbaya ya usalama.

Kwa kuidhinishwa Sudan Kusini kuwa mwakachama wa 6 wa EAC, jumuiya hiyo sasa imekuwa na idadi jumla ya watu milioni 162. Mbali na Sudan Kusini, nchi wanachama wengine ni Kenya, Tanzania, Rwanda, Burundi na Uganda.

Tags