IOM yaomba ufadhili wa dola milioni 81 kwa ajili ya Afrika Mashariki
Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) na washirika 45 wa masuala ya kibinadamu na kimaendeleo wameiomba jamii ya kimataifa msaada wa dola milioni 81 kwa ajili ya kuokoa maisha kwa zaidi ya wahamiaji milioni moja wakiwemo wanawake na watoto na jumuiya zinazowahifadhi katika nchi za Djibouti, Ethiopia, Somalia, Tanzania, Kenya na Yemen.
Wito huo umetolewa ndani ya mfumo wa mpango wa kukidhi mahitaji ya wimbi la wahamiaji kutoka Pembe ya Afrika kwenda Yemen na Afrika Kusini, unaoratibiwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji.
Kwa mujibu wa shirika hilo, mamia ya maelfu ya wahamiaji kila mwaka hufanya safari hatari zisizo za kawaida, haswa kutoka Ethiopia na Somalia, kuelekea katika nchi za Ghuba ya Uajemi kama Saudi Arabia kupitia Djibouti na Yemen. Wahamiaji wengine huchukua njia mbadala kupitia Kenya na Tanzania kuelekea Afrika Kusini.
Wahajiri hao huchukua uamuzi wa kuacha nchi zao kwa ajili ya kusaka nafasi za kazi kutokana na umaskini uliokithiri na hali ngumu ya kiuchumi, pamoja na kukimbia ghasia na machafuko ya kisiasa. Athari mbaya za majanga ya hali ya hewa pia zinazidi kuwa kichocheo kikuu cha uhamiaji katika eneo hilo la Afrika.
Kwa mujibu wa Kituo cha Data cha Kanda cha IOM, harakati 446,000 zilirekodiwa katika njia ya mashariki mwaka jana, 10% ikihusisha watoto. Wahamiaji hao mara nyingi hukabiliwa na hatari za maisha kama vile njaa na ukosefu wa maji.

Takwimu za baadhi ya mashirika ya kimataifa zinaonyesha kuwa, takriban watu 559 walipoteza maisha katika njia za mashariki na kusini mwaka jana, 2024, na kwamba idadi ya vifo visivyoripotiwa inaaminika kuwa kubwa zaidi.
Wanawake na wasichana wanawakilisha takriban theluthi moja ya harakati zilizorekodiwa za wahamiaji hao, ambao huwa katika hatari kubwa ya ukatili wa kingono na unyanyasaji kijamii.