Watu 70 hawajulikani waliko baada ya boti kuzama mkoani Kasai, DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133394-watu_70_hawajulikani_waliko_baada_ya_boti_kuzama_mkoani_kasai_drc
Watu wapatao 70 hawajulikani walipo baada ya boti kuzama mtoni katika Mkoa wa Kasai katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2025-11-20T09:10:15+00:00 )
Nov 20, 2025 06:09 UTC
  • Watu 70 hawajulikani waliko baada ya boti kuzama mkoani Kasai, DRC

Watu wapatao 70 hawajulikani walipo baada ya boti kuzama mtoni katika Mkoa wa Kasai katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumatano na Redio ya Umoja wa Mataifa, boti hiyo ilikuwa ikielekea mji mkuu, Kinshasa ikitokea bandari ya Bena Dibele, iliyoko umbali wa zaidi ya kilomita 800 (maili 497), wakati ilipozama siku ya Jumatatu katika Mto Sankuru kutokana na vimbunga.

"Boti hiyo ilikuwa imebeba karibu watu 120. Watu wapatao 50 wameokolewa hadi sasa, na juhudi za utafutaji zinaendelea kwa wale waliopotea," ilieleza ripoti hiyo ikimnukuu msimamizi wa eneo hilo Francois Ahoka.

Ahoka ameashiria ugumu zinaokabiliana nao timu za uokoaji na kutoa wito kwa familia kuwasiliana na mamlaka za mitaa kwa ajili ya kuwatambua manusura na miili iliyopatikana.

Usafiri wa majini ni jambo la kawaida nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na tatizo la barabara nyingi mbovu ambazo hazipitiki.

Ajali za majini zinazosababisha maafa ya roho za watu zimekuwa zikiripotiwa mara kwa mara katika nchi hiyo.

Katikati ya mwezi Septemba mwaka huu, watu wapatao 193 walifariki dunia katika matukio mawili ya kuzama boti yaliyotokea tarehe 10 na 11 kwenye maeneo ya kaskazini-magharibi mwa jimbo la Equateur.../