Uchaguzi Mkuu unakaribia Uganda, Polisi wazuia wapinzani kufanya kampeni Arua
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133404-uchaguzi_mkuu_unakaribia_uganda_polisi_wazuia_wapinzani_kufanya_kampeni_arua
Huku Uchaguzi Mkuu ukizidi kukaribia nchini Uganda, Jeshi la Polisi la nchi hiyo limekizuia chama cha upinzani cha Jukwaa la Umoja wa Kitaifa NUP kuingia katika eneo la kampeni za uchaguzi lililokuwa limepangwa kabla kwenye mji muhimu wa Arua wa kaskazini mwa Uganda jana Jumatano.
(last modified 2025-11-20T10:16:02+00:00 )
Nov 20, 2025 10:16 UTC
  • Uchaguzi Mkuu unakaribia Uganda, Polisi wazuia wapinzani kufanya kampeni Arua

Huku Uchaguzi Mkuu ukizidi kukaribia nchini Uganda, Jeshi la Polisi la nchi hiyo limekizuia chama cha upinzani cha Jukwaa la Umoja wa Kitaifa NUP kuingia katika eneo la kampeni za uchaguzi lililokuwa limepangwa kabla kwenye mji muhimu wa Arua wa kaskazini mwa Uganda jana Jumatano.

Wafuasi wa chama cha NUP walikuwa wamekusanyika na kujiandaa vizuri kumkaribisha mgombea urais wa chama hicho Bobi Wine, ambaye anaendelea na kampeni zake za nchi nzima kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Januari 2026.

Uchuguzi Mkuu wa mwezi Januari 2026 utatoa fursa kwa wananchi wa Uganda kuchagua Rais, Wabunge, madiwani na serikali za mitaa. Rais Yoweri Museveni, ambaye ametawala tangu mwaka 1986, ameidhinishwa tena na tume ya uchaguzi kugombea muhula mwingine na hivyo kuufanya uchaguzi ujao kuwa na mchuano mkali.

Hata hivyo, hatokuwepo mgombea mkongwe wa upinzani Dk. Kizza Besigye ambaye hivi sasa yuko kizuizini kwa zaidi ya mwaka mmoja. Mkewe Daktari Besigye yaani Bi Winnie Byanyima, ametoa ombi la hisia kali la kutaka kuachiliwa huru mumewe huku Besigye mwenyewe na wafuasi wake wakihoji, ni kitu gani serikali ya Rais Museveni inakiogopa kutoka kwa Besigye wakati kwa mujibu wa serikali yenyewe ya Uganda, tishio kubwa kwa Museveni wakati wa uchaguzi ujao ni Bobi Wine, si Besigye.

Besigye na msaidizi wake walikamatwa jijini Nairobi mwezi Novemba 2024, wakarudishwa Uganda, na kupelekwa moja kwa moja gerezani kwa mashtaka ya uhaini. Kesi yao iliyopelekwa kwenye Mahakama ya Kijeshi iliangushwa na hukumu ya Mahakama Kuu iliyosema kuwa Mahakama ya Kijeshi haipaswi kuendesha kesi ya raia. Wawili hao sasa wana mashtaka ya uhaini mbele ya Mahakama Kuu.