Wanawake wajawazito Sudan wafanya safari ngumu za kukimbia machafuko ya El-Fasher
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133400-wanawake_wajawazito_sudan_wafanya_safari_ngumu_za_kukimbia_machafuko_ya_el_fasher
Nadra Mohamed Ahmed alikuwa na ujauzito wa miezi saba wakati alipokimbia machafuko na mauaji katika mji wake wa El-Fasher nchini Sudan. Baada ya kutembea kwa karibu kilomita 40 katika barabara zisizo salama na watoto wake wawili, alipata usafiri salama hadi kwenye makazi yake mapya.
(last modified 2025-11-20T10:14:55+00:00 )
Nov 20, 2025 10:14 UTC
  • Wanawake wajawazito Sudan wafanya safari ngumu za kukimbia machafuko ya El-Fasher

Nadra Mohamed Ahmed alikuwa na ujauzito wa miezi saba wakati alipokimbia machafuko na mauaji katika mji wake wa El-Fasher nchini Sudan. Baada ya kutembea kwa karibu kilomita 40 katika barabara zisizo salama na watoto wake wawili, alipata usafiri salama hadi kwenye makazi yake mapya.

"Nilipofika hapa, nilikuwa nimepoteza damu nyingi," amesema Nadra Ahmed kutoka kwenye hema lake katika kambi iliyojaa wakimbizi katika mji wa Al-Dabbah, kaskazini mwa Sudan. "Nililazwa katika ICU ambapo nilikaa siku kadhaa nikiongezewa damu."

Mwanamke huyo alifika kambini hapo miezi miwili kabla ya mji wa El-Fasher kutekwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF, kundi ambalo limekuwa likipigana na jeshi la Sudan SAF kwa zaidi ya miaka miwili. Zaidi ya wanawake wajawazito 140 wameshafika katika kambi za Al-Dabbah mji wa El-Fasher ulipotekwa na RSF mwezi uliopita.

Maafisa mbalimbali wa masuala ya wakimbizi wanasema kuwa wengi wa wanawake hao huwa wanafika kenye kambi hiyo wakiwa wamepata matatizo makubwa, yaani kutokwa na damu nyingi, ambapo wakati mwingine huishia katika kuharibika mimba zao. Akiwa amembeba mgongoni binti yake wa miaka minne na kumshika mkono mwanawe mdogo wa miaka sita, Nadra Ahmed anasema alilazimika kuingia safarini na kutembelea kwa muda wa siku 14 bila ya kuwa na mumewe ambaye walipoteana muda mfupi kabla ya kukimbia El-Fasher.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa, Bi Nadra ni mmoja wa wanawake wengi wajawazito wa Sudan ambao wanapambana kukamilisha miezi yao ya kujifungua watoto wenye afya njema, katika nchi ambayo asilimia 80 ya vituo vya matibabu vimeharibiwa kabisa. Wiki iliyopita, Anna Mutavati, Mkurugenzi wa Kanda ya Wanawake wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya maeneo ya mashariki na kusini mwa Afrika aliwaambia waandishi wa habari kwamba wanawake wa Sudan wanalazimika kujifungulia mitaani kutokana na kusambaratika mfumo wa afya nchini humo.