Kharrazi amwambia Trump: Huwezi kuilazimisha Iran kufumbia macho haki zake
Kamal Kharrazi, mshauri wa ngazi za juu wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametoa ujumbe wa wazi kwa Marekani na kusema kuwa, siasa za Donald Trump za kutumia mabavu haziwezi kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kubadilisha njia yake.
Kamal Kharrazi amesema hayo katika mahojiano ya kina aliyofanyiwa na televisheni ya CNN na kusisitiza kuwa: "Wamejaribu kutumia mabavu, na sasa wanaelewa kuwa siasa zao za kutumia mabavu hazifanyi kazi."
Amegusia mabavu yaliyotumiwa na Marekani dhidi ya Iran katika kipindi cha miongo kadhaa iliyopita na kuongeza kuwa, kama Trump anadhani kuwa anaweza kulilazimisha taifa la Iran libadilishe msimamo wake atambue kuwa yuko kwenye makosa makubwa, hawezi kuisukuma Jamhuri ya Kiislamu kuacha njia yake sahihi.
Amegusia pia namna Marekani ilivyoungana na utawala wa Kizayuni kuanzisha na kuendesha vita vya kivamizi na kichokozi dhidi ya Iran mwezi Juni mwaka huu na kushambulia mpaka vituo vya nyuklia nchini Iran lakini amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kubakia imara kikamilifu na imejiandaa vilivyo kukabiliana na mzozo wowote, iwe ni kutoka kwa Marekani au kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wakati huo huo lakini amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaendelea kunyoosha mkono wa utatuzi wa kidiplomasia wa masuala mbalimbali lakini kwa sharti jambo hilo lifanyike kwa msingi wa kuheshimiana, usawa na kwa mujibu wa ajenda iliyokubaliwa awali, masharti ambayo Marekani bado haijayatimiza.
Mshauri huyo Kkiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameupa nasaha utawala wa Trump akiutaka uanze kufuata njia sahihi kuhusu Iran akisema kwamba, hatua yoyote ya maana itapokewa vizuri na Tehran, lakini kwa sharti Marekani iache siasa zake za kibeberu, vitisho na mashinikizo.