Mgogoro wa Sahel: Tishio la Kikanda au Hatari ya Kimataifa?
-
Ukanda wa Sahel barani Afrika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ametahadharisha kuhusu ukuaji na upanukaji wa makundi ya kigaidi barani Afrika na kutangaza kuwa: "Hali ya usalama, hasa katika Afrika Magharibi na eneo la Sahel, inazidi kuwa mbaya siku hadi siku."
Antonio Guterres amesema: "Tunakabiliwa na hatari ya athari mbaya katika eneo lote la Sahel. "Nchi nyingi zinayumbayumba," amesema Guterres na kuongeza kuwa dunia inahitaji kushikamana na watu wa eneo la Sahel.
Akisisitiza kwamba ugaidi katika eneo la Sahel si tukio la kikanda tu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema: "Muungano wa makundi ya kigaidi barani Afrika na kwingineko umeyageuza makundi haya kuwa tishio linaloongezeka duniani."
Eneo la Sahel ni ukanda mkubwa wa kijiografia barani Afrika uliopo kati ya Jangwa la Sahara huko kaskazini mwa Afrika, na maeneo ya kitropiki ya kusini mwa bara hilo, ukijumuisha maeneo ya kaskazini mwa Senegal, kusini mwa Mauritania, Mali, Burkina Faso, kusini mwa Algeria, Niger, Chad, kaskazini mwa Sudani Kusini, Sudan na Eritrea.
Ingawa Afrika, hasa eneo la Sahel, imekuwa ikikumbwa na machafuko yanayosababishwa na makundi ya kigaidi, matukio ya hivi karibuni katika uwanja wa kimataifa na hali ya kikanda pia yamechochea uwepo na harakati za makundi hayo; kama anavyotahadhariisha Guterres kwamba sasa, ugaidi barani Afrika si tishio la kikanda pekee, bali linabadilika kwa kasi kubwa na kuwa hatari ya kimataifa.
Hapa linajitokeza swali kwamba, kwa nini makundi ya kigaidi yanaongezeka barani Afrika? Ukuaji wa makundi haya unaweza kuchunguzwa katika nyanja kadhaa za usalama, masuala ya kibinadamu, kiuchumi na kisiasa.
Kwa mtazamo wa usalama, eneo la kijiografia la Sahel na udhaifu wa serikali kuu za nchi katika eneo hilo vimetayarisha mazingira yanayofaa kwa makundi ya kigaidi kufanya harakati zao katika maeneo hayo. Makundi yanye mfungamano na al-Qaeda, ISIS na Boko Haram yamejiimarisha sana katika eneo hilo. Makundi hayo yamefanya hali kuwa hatari na ngumu zaidi kwa wakazi wa eneo hilo kwa kushambulia misafara ya kijeshi, kuteka nyara watu na kuwaua raia, na vilevile kwa kusababisha ukosefu wa usalama katika njia muhimu za usambazaji wa mafuta na bidhaa muhimu na kuvuruga usambazaji wa nishati, kama ilivyotokea hivi karibuni nchini Mali. Kwa upande mwingine, mafungamano ya kimataifa ya makundi haya yanaonyesha kwamba shughuli zao haziishii katika sehemu hiyo ya Afrika, bali zinafanyika katika mtandao mpana zaidi.
Madhaya ya binadamu ya mgogoro huu yanazidi vipimo vyake vya usalama. Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, takriban watu milioni 4 wameyakimbia makazi yao katika nchi za Burkina Faso, Mali, Niger na nchi nyingine jirani kutokana na harakati za kigaidi za makundi hayo. Zaidi ya shule 14,000 na vituo vya afya 900 vimefungwa na kuwaacha mamilioni ya watu wakikosa huduma za kielimu na kimatibabu. Ukosefu wa huduma hizo unakifanya kizazi kipya kikabiliwe na mustakabali wa giza na kutengeneza umaskini, ujinga wa kutojua kusoma na kuandika, na kukata tamaa - hasa katika nchi za Kiafrika-; suala ambalo lenyewe pia huwa sababu ya kuajiriwa vijana katika makundi ya kigaidi, ambayo huwaahidi misaada ya kifedha na hali bora.
Sababu nyingine ya ukuaji wa makundi ya kigaidi barani Afrika ni ushindani wa chini kwa chini na wa waziwazi kati ya mataifa yenye nguvu ya kikanda na kimataifa, ikiwa ni pamoja na uwepo wa kijeshi na kiuchumi wa nchi mbalimbali barani humo. Nchi hizo zimezidisha ukosefu wa usalama katika eneo hilo kwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi kwa siri, na wakati mwingine kuyapa misaada ya kifedha na kijeshi ili kuhalalisha uwepo wao kwenye maeneo yenye migogoro ya Afrika. Ukweli ni kwamba, badala ya kushirikiana kupambana na ugaidi, mataifa mengi hasimu ya kigeni yanajihusisha na ushindani wa kupata ushawishi na maslahi zaidi ya kiuchumi barani Afrika; hali ambayo si tu imesababisha kufeli juhudi za kudhibiti ugaidi, lakini pia imefungua njia ya kupanuka harakati za makundi yenye silaha.
Kwa upande mwingine, mabadiliko ya hali ya hewa pia yamechangia pakubwa katika kuenea kwa ugaidi. Nchi za Sahel zinasumbuliwa na umaskini mkubwa, taasisi dhaifu na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi. Ukame, kupanuka jangwa na kupungua kwa maliasili kumezidisha ushindani wa kupata rasilimali chache za dunia na kufungua njia ya kuongezeka migogoro na mapigano ya ndani.
Mambo haya yote yanaonyesha kwamba, ukuaji wa ugaidi barani Afrika sasa umekuwa hatari kubwa si tu kwa nchi za bara hilo, bali pia kwa dunia nzima. Hivyo basi, mapambano ya kukabiliana na tishio hili yanahitaji hatua mseto za kiusalama pamoja na msaada wa kifedha na kibinadamu, kuimarisha taasisi za serikali, kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa na kutayarisha fursa za maendeleo kwa watu wa eneo hilo.
Katika hali hii, iwapo hii leo dunia itapuuza mgogoro wa Sahel, kesho italazimika kukabiliana na wimbi la kimataifa la ukosefu wa usalama, uhamaji mkubwa wa watu na vurugu zisizoisha. Ugaidi barani Afrika si onyo tu, bali ni tishio tarajiwa ambalo, bila kuwepo ushirikiano na ushiriki wa nchi mbalimbali, litahatarisha sana maeneo mengi ya dunia. Mustakabali wa Afrika ni mustakabali wa dunia, na kuchelewa kuchukua hatua kutakuwa na gharama kubwa kwa ubinadamu.