Ubepari wa Magharibi na Kuporomoka kwa Maadili
Ubepari katika jamii za Magharibi, na msisitizo wake juu ya faida ya mtu binafsi na kutenganisha maadili na uchumi, umesababisha madhara makubwa na matokeo mabaya sana kwa maadili ya binadamu.
Matokeo mabaya ya mienendo ya kibepari ya Magharibi kuhusu kutanguliza mbele maslahi ya mtu binafsi na msisitizo wa kupata faida za kibinafsi, bila kujali njia zinazotumiwa kupata faida hiyo, na hatimaye kutenganisha baina ya maadili na uchumi, ni pamoja na mambo kama vile ubinafsi uliokithiri, kudhoofisha mshikamano wa kijamii, kuenea vurugu na machafuko na kupuuzwa maadili.
Mojawapo ya ukosoaji muhimu zaidi dhiidi ya ubepari wa Magharibi ni ule unaosema kuwa mwanadamu wa leo amebadilika na kuwa "mwanadamu wa kiuchumi"; kwa maana ya kiumbe anayetenda kwa msingi wa faida binafsi na mahesabu ya faida na hasara tu. Kwa mtazamo huu, maadili yametenganishwa na uchumi, na maadili ya kibinadamu kama vile uadilifu, huruma na kujitolea hayana nafasi katika uchukuaji wa maamuzi ya kiuchumi. Utenganisho huu -baina ya maadili na uchumi- hufanya faida ya mtu binafsi kuwa kigezo kikuu cha mienendo ya mwanadamu, badala ya kutaka kheri na mema kwa ajili ya watu wote; na matokeo yake, mahusiano ya kibinadamu yanafifizwa na kuwa mahusiano ya kiwenzo na yenye mwelekeo wa faida na maslahi ya kibinafsi.
Uchunguzi umeonyesha kwamba, mgogoro wa kimaadili uliopo katika mfumo wa kibepari wa Magharibi umesababisha ongezeko la ukatili na mienendo ya kufurutu mipaka katika jamii za Magharibi, hasa Marekani. Kwa sababu, wakati maadili yanaposahaulika na kufunikwa na mienendo ya kujinufaisha kibinafsi, jamii huelekezwa kwenye ushindani usio na huruma na wa kikatili wa kila mtu kutaka kumfuta na kummaliza msindani wake. Hali hii si tu kwamba inafanya mahusiano ya kijamii kuwa dhaifu, lakini pia huchochea utamaduni wa watu kuwa makatili na kutoaminiana kwa umma.
Ubepari wa Magharibi pia umechangia sana katika kuunda ubinafsi uliokithiri kwa kusisitiza ubinafsi (Individualism) yaani kutanguliza mbele thamani au nafasi kuu ya mtu binafsi kuliko jamii. Katika hali kama hii, watu hutaka kutimiza maslahi yao binafsi badala ya kufikiria majukumu yao ya kijamii. Jambo hili hudhoofisha mshikamano wa kijamii, kupunguza hali ya kuaminiana baina ya umma na kuwafanya watu wapuuze matatizo ya wanadamu wenzao. Matokeo yake ni kutoweka maadili kama vile ushirikiano, muawana na uadilifu wa kijamii ambavyo nafasi yao huchukuliwa na ushindani usio na mwisho na kujipatia maslahi na faida za kibinafsi.
Matokeo mengine ya ubepari wa Magharibi ni kukithiri unuzi wa huduma na ulaji wa bidhaa bila ya kusita (consumerism). Katika mfumo huu, watu hujihusisha zaidi na kununua na kutumia bidhaa mpya kuliko ustawi wa kiroho na kimaadili. Mtindo huu wa maisha wa homa ya kujishughulisha zaidi na ununuzi na utumiaji bidhaa mpya si tu kwamba husababisha uharibifu wa mazingira na maliasili, lakini pia hupunguza na kushusha chini kabisa maadili ya binadamu; na thamani ya wanadamu hupimwa kwa mujibu wa kiasi cha mali na matumizi yao, si kwa maadili au sifa zao za kiroho.
Katika mfumo wa kibepari wa Magharibi, uchumi hufafanuliwa kama uwanja uliojitenga na maadili. Mtengano huu huwa sababu ya kuchukuliwa maamuzi ya kiuchumi bila kujali matokeo yake mabaya kwa maadili. Kwa mfano, makampuni yanaweza kutumia vibaya nguvu kazi, kuharibu mazingira au kuzalisha bidhaa zenye madhara ili kuongeza faida, bila kukubali kubeba majukumu na uwajibikaji wa kimaadili kwa vitendo kama hivyo. Mienendo kama hiyo huweka kando maadili na kuwatumbukiza wanadamu katika duara lisilo na mwisho la ushindani wa kujipatia faida sambamba na kukanyaga maadiili na sifa nyingine za kibinadamu.
Mwishowe, ni lazima isemwe kwamba, ubepari katika jamii za Magharibi, umekuwa na matokeo mabaya sana kwa maadili ya binadamu kutokana na msisitizo wake juu ya faida za mtu binafsi (ubinafsi au Individualism), unuzi wa huduma na ulaji wa bidhaa bila ya kusita (consumerism), na kutenganisha maadili na uchumi. Matokeo hayo ni pamoja na ubinafsi uliokithiri, kuporomoka kwa mshikamano wa kijamii, kuenea kwa ukatili, ufuska na utovu wa maadili na kutojali thamani za binadamu.
Katika hali kama hii, upo udharura wa kufikiria upya uhusiano kati ya maadili na uchumi na kurudi kwenye maadili ya kibinadamu kama vile uadilifu, kuwa na huruma na uwajibikaji wa kijamii.