Waasi wa RSF wameharibi viwanda zaidi ya 1,800  huko Khartoum, Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133428-waasi_wa_rsf_wameharibi_viwanda_zaidi_ya_1_800_huko_khartoum_sudan
Waziri wa Viwanda na Biashara wa Sudan, Mahasen Ali Yaqoub, amesema  kuwa zaidi ya viwanda 1,800 vimeharibiwa na kundi la waasi wa Rapid Support Forces (RSF) katika jimbo la Khartoum.
(last modified 2025-11-21T07:59:50+00:00 )
Nov 21, 2025 07:59 UTC
  • Waasi wa RSF wameharibi viwanda zaidi ya 1,800  huko Khartoum, Sudan

Waziri wa Viwanda na Biashara wa Sudan, Mahasen Ali Yaqoub, amesema  kuwa zaidi ya viwanda 1,800 vimeharibiwa na kundi la waasi wa Rapid Support Forces (RSF) katika jimbo la Khartoum.

Akizungumza Alhamisi, Yaqoub amesema: “Kikundi cha waasi kimeharibu viwanda 1,877 katika Jimbo la Khartoum, vikiwemo 553 vilivyoharibiwa kabisa na 1,267 kwa sehemu.

Katika kikao na na waandishi wa habari mjini Port Sudan waziri huyo ameongeza kuwa, uchunguzi wa uharibifu uliofanywa na serikali baada ya kurejesha udhibiti wa Khartoum kutoka kwa waasi ulionyesha kiwango kikubwa cha uharibifu.

Aidha amebainisha kuwa mashambulizi mengi ya waasi wa RSF yalilenga miundombinu ya viwanda, hususan vifaa na mifumo ya nishati, ili kuzuia kuanza tena kwa shughuli za uzalishaji katika mji mkuu.

Yaqoub ameongeza kuwa: “Sekta ya viwanda imekumbwa na uharibifu mkubwa na wa kimfumo, hali iliyosababisha kusitishwa kabisa kwa uzalishaji katika Khartoum, Al-Jazira na Sennar."

Amesisitiza kuwa mashambulizi ya waasi wa RSF “yamelemaza kabisa sekta ya viwanda” nchini Sudan, na kulazimisha taifa kuagiza mahitaji yake ya msingi kutoka nje.

Mnamo Mei 2025, jeshi la Sudan lilitangaza kurejesha udhibiti kamili wa jimbo la Khartoum.

Jeshi na waasi wa RSF wamekuwa wakipigana vita vya maangamizi tangu Aprili 15, 2023, vita ambavyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya raia na kupelekea karibu watu milioni 14 kuyahama makazi yao.

Serikali ya Sudan inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kuunga mkono waasi hao wa RSF wanaotekeleza ukatili na mauaji ya kimbari nchini humo.

Hadi sasa, RSF inadhibiti majimbo yote matano ya Darfur magharibi mwa Sudan, huku jeshi likishikilia majimbo 13 yaliyosalia kusini, kaskazini, mashariki na katikati, yakiwemo mji mkuu, Khartoum.