Iran yalaani azimio la IAEA kuhusu mpango wake wa nyuklia
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani vikali azimio lililopitishwa na Bodi ya Magavana wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), ikilitaja kuwa “batili na lisilo na msingi.”
Bodi hiyo, siku ya Alhamisi, ilipitisha azimio lililoandaliwa na Troika ya Ulaya yaani Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, pamoja na Marekani, kwa kura 19 za ndio na 3 la huku wajumbe 12 wakijizuia kupiga kura. Azimio hilo linaitaka Tehran “bila kuchelewa” kutoa ripoti kuhusu akiba ya madini ya urani iliyorutubishwa na miundombinu iliyoharibiwa katika mashambulizi ya Juni yaliyofanywa na Israel na Marekani, huku likipuuzia ushirikiano wa muda mrefu wa Iran na shirika hilo.
Katika taarifa yake, wizara imesema hatua hiyo inathibitisha kuwa Marekani na Troika ya Ulaya wanatumia vibaya shirika hilo ili kuongeza shinikizo dhidi ya Iran. Wizara iliongeza kuwa takribani nusu ya wanachama wa IAEA, wakiwemo wajumbe wawili wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, walikataa azimio hilo.
Wizara ilisisitiza kuwa azimio hilo linakiuka misingi ya Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT), unaotoa haki kwa wanachama kutumia nishati ya nyuklia kwa madhumuni ya amani. Aidha, ilibainisha kuwa Baraza la Magavana halina mamlaka ya kufufua maazimio ya Baraza la Usalama yaliyokwisha muda wake, na kulihusisha kitendo cha Marekani na washirika wake wa Ulaya na “nia mbaya” na mwenendo usio na uwajibikaji.
Zaidi ya hayo, wizara ilionya kuwa msisitizo wa kurudia hatua kama hizo unaweza kusababisha mkanganyiko wa kisheria na kuongeza mgawanyiko ndani ya taasisi za kimataifa, jambo litakalodhoofisha misingi ya utaratibu wa kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia. Wizara ilisisitiza kuwa Iran haijawahi kujaribu kutengeneza silaha za nyuklia, na badala yake ikataja Israel na silaha zake za nyuklia kama tishio kuu kwa amani na usalama wa kimataifa.
Wizara pia ilibainisha kuwa Marekani na mataifa matatu ya Ulaya wanashirikiana na uhalifu wa Israel katika eneo kwa kupuuza hatari ya utawala huo na kujaribu kuilaumu Iran kwa mpango wake wa nyuklia wenye malengo ya amani.
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi amesema kuwa Iran sasa inachukulia makubaliano ya Cairo na IAEA kuwa yamefutwa, kufuatia kupitishwa kwa azimio la kupinga Iran katika Bodi ya Magavana.
Araghchi amelaani hatua hiyo, akilitaja azimio hilo kuwa “batili na lisilo na msingi.” Amesema kuwa azimio hilo lilipitishwa “kwa shinikizo kutoka mataifa hayo manne” licha ya upinzani au kujizuia kwa wajumbe 15 wa baraza.
Araghchi ameongeza kuwa kitendo hicho kimepunguza “heshima na uhuru” wa IAEA na kitavuruga ushirikiano wa shirika hilo na Iran.