Watoto wa Kipalestina katika jahanamu ya jela za Israel
-
watoto 350 wa Kipalestina wanashikiliwa katika magereza za Israel
Jana, tarehe 20 Novemba, dunia iliadhimisha"Siku ya Watoto Duniani," huku hali ya mambo huko Palestina ikionyesha picha tofauti kabisa, ambapo watoto ndio wanaoongoza katika janga linaloendelea kulitesa eneo la Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za taasisi za Palestina, watoto 350,000 katika Ukanda wa Gaza wako hatarini kufa kwa sababu ya njaa kutokana na ukosefu wa chakula, na watoto wachanga 40,000 wanakabiliwa na hatari hiyo hiyo kutokana na uhaba wa maziwa ya watoto.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza inasema, watoto 20,000 wameuawa shahidi katika kipindi cha miaka miwili ya mauajii ya kimbari ya Israel, na zaidi ya watoto 56,000 wamekuwa yatima, wakipoteza mzazi mmoja au wote wawili, huku zaidi ya watoto 5,100 wakihitaji kupelekwa nje ya nchi haraka kwa ajili ya kupewa matibabu ya kuokoa maisha yao.
Mkuu wa Klabu ya Wafungwa wa Palestina, Abdullah Al-Zaghari, anasema kwamba watoto wa Palestina "wanaishi katika kipindi cha umwagaji damu zaidi ambacho Palestina imekuwa ikipitia kwa miongo kadhaa," akisisitiza kwamba uhalifu wa kimatibabu na uhalifu wa kutesa watu kwa njaa umemfanya mtoto wa Palestina "kuwa mwathirika wa mauaji yanayoendelea kufanywa na utawala vamizi kwa msaada wa baadhi ya nchi za Magharibi."
Abdullah Al-Zaghari anasema kwamba katika Ukanda wa Gaza, watoto hawatafuti tena elimu au michezo, bali "kila asubuhi wanatafuta maji, chakula au mahali pa kujisaidia," akieleza kuwa nchi za Magharibi, ambazo hutoa mabilioni ya dola kusiaidia Israel, "haziwezi kuwapa maji, dawa na matibabu" maelfu ya watoto waliozingirwa wa Palestina.
Mkuu wa Klabu ya Wafungwa wa Palestina amesema kwamba watoto wachanga walio chini ya majivu na vifusi vya nyumba zilizoharibiwa kwa mabomu ya Israel ni sehemu ya "janga halisi" ambalo ulimwengu unalitazama kwa macho tu bila kuchukua hatua, kwani "miili yao bado inashikiliwa na wavamizi."
Ni vyema kukumbusha hapa kuwa takriban watoto 350 wa Kipalestina, wakiwemo wasichana wawili, kwa sasa wanashikiliwa katika magereza ya Israel katika hali zinazokiuka viwango vya kimataifa vya ulinzi wa watoto, huku zaidi ya watoto 90 wakikabiliwa na kifungo cha kiutawala, ikiwa na maana ya kushikiliwa bila kufunguliwa mashtaka.