The Guardian: Israel imetumia mabomu yaliyopigwa marufuku dhidi ya Lebanon
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i133440-the_guardian_israel_imetumia_mabomu_yaliyopigwa_marufuku_dhidi_ya_lebanon
Uchunguzi mpya uliofanywa na gazeti la Uingereza, The Guardian, umebaini kuwa Israel ilitumia mabomu yaliyopigwa marufuku wakati wa vita vyake vya hivi karibuni dhidi ya Lebanon.
(last modified 2025-11-21T09:57:26+00:00 )
Nov 21, 2025 09:57 UTC
  • Bomu la Vishada
    Bomu la Vishada

Uchunguzi mpya uliofanywa na gazeti la Uingereza, The Guardian, umebaini kuwa Israel ilitumia mabomu yaliyopigwa marufuku wakati wa vita vyake vya hivi karibuni dhidi ya Lebanon.

Gazeti hilo limeeleza kwamba picha za kipekee - ambazo lilizishuhudia na kuzithibitisha - zinaonyesha kwamba Israel ilitumia mabomu ya vishada katika vita vya miezi 13 dhidi ya Lebanon; huo ukiwa ushahidi wa kwanza wa kutumiwa silaha hizo tangu vita vya 2006.

Picha hizo, ambazo zimechunguzwa na wataalamu sita wa silaha kutoka taaluma tofauti, zimeonyesha mabaki ya aina mbili tofauti za mabomu ya vishada ya Israel, yaliyopatikana katika maeneo matatu tofauti kusini mwa Mto Litani katika mabonde yenye misitu, ikiwa ni pamoja na Bonde la Zibqin, Bonde la Barghaz na Bonde la Deir Siryan.

Gazeti hilo limeeleza kwamba miongoni mwa wataalamu waliothibitisha picha za kwanza za mabomu ya vishada yaliyopigwa marufuku yaliyotumiwa na jeshi la Israel huko Lebanon ni Brian Kastner, mkuu wa utafiti wa migogoro katika Amnesty International, na Jensen Jones, mkurugenzi wa kampuni ya Huduma za Utafiti wa Silaha kwa Ajili ya Ushauri wa Kiupelelezi.

Mabomu ya vishada ni hatari sana kwa maisha ya raia

Mbali na kuwa ufichuzi huu unahesabiwa kuwa dalili ya kwanza kwamba Israel imetumia mabomu hayo yaliyopigwa marufuku tangu miongo miwili iliyopita, hii ni mara kwanza Israel kutambulishwa kuwa imetumia aina mbili mpya za mabomu ya aina hiyo ambayo ni kombora la 155mm M999 Barak Eitan lililotengenezwa na kampuni ya Israel, Elbit Systems, na kombora la 227mm Ra’am Eitan.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Guardian, mabomu haya hubeba vijibomu kadhaa vidogo ambavyo huangushwa juu ya eneo kubwa sawa na viwanja kadhaa vya mpira wa miguu.

Mabomu haya ya vishada yamepigwa marufuku kwa sababu takriban 40% ya vijibomu vyake vidogo hushindwa kulipuka, na hivyo kuhatarisha maisha ya raia wanapoingia kwenye eneo lenye silaha za aina hiyo.

Gazeti hilo la Uingereza limesema kwamba Lebanon inakabiliwa na mabaki ya mabomu ya vita vya 2006, kwani maelfu ya mabomu ambayo hayajalipuka bado ni tishio kwa raia.