Cuba: Marekani inataka kuivamia kijeshi Venezuela kwa visingizio vya uongo
-
Cuba: Marekani inataka kuivamia kijeshi Venezuela kwa visingizio vya uongo
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba amelaani vikali hatua za Marekani za kuhalalisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Venezuela.
Bruno Rodríguez Parrilla Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba amesisitiza katika ujumbe uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X: "Tunalaani uwongo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, ambayo, chini ya uongozi wa Waziri fisadi na mwongo Marco Rubio, inajaribu kuhalalisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Venezuela kwa kisingizio cha uongo."
Aliongeza kuwa Washington, "kwa msaada wa vyombo vya habari, inataka kurekebisha na kuhalalisha uchokozi dhidi ya taifa huru mbele ya kila mtu." Rodriguez alisema wanajaribu kumhusisha Rais halali wa Venezuela, Nicolas Maduro, katika biashara ya dawa za kulevya na ugaidi kwa njia isiyo sahihi.
Katika kile kinachotafsiriwa kama harakati ya kibeberu na ya kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine, hivi karibuni Rais wa Marekani Donald Trump aliashiria kuwa siku za Rais Nicolas Maduro wa Venezuela kuweko madarakani zinakaribia ukingoni, huku mvutano kati ya nchi hizo mbili ukiwa unaongezeka sambamba na Washington kushamirisha kuwepo kwake kijeshi katika eneo la Carribean.
Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani viliripoti kuwa serikali ya Trump imeamua kufanya mashambulio dhidi ya vituo vya kijeshi nchini Venezuela kama sehemu ya vita vyake vinavyodaiwa kuwa ni dhidi ya "ugaidi wa madawa ya kulevya" na kwamba mashambulizi hayo yanaweza kutokea wakati wowote ule kutoka sasa.
Taasisi za kutetea haki za binadamu na wataalamu wa sheria wamehoji na kukosoa uhalali wa operesheni hizo za kijeshi, wakisema kwamba mashambulizi ya Marekani kwenye boti zinazodaiwa kubeba mihadarati yanakiuka sheria za kimataifa.