Marekani na nchi tatu za Ulaya zimeuaje Mkataba wa Cairo?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i133484-marekani_na_nchi_tatu_za_ulaya_zimeuaje_mkataba_wa_cairo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika kwenye akaunti yake ya X kwamba: ""Mkataba wa Cairo" umeangamizwa na Marekani na nchi tatu za Ulaya."
(last modified 2025-11-23T02:30:50+00:00 )
Nov 23, 2025 02:30 UTC
  • Marekani na nchi tatu za Ulaya zimeuaje Mkataba wa Cairo?

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameandika kwenye akaunti yake ya X kwamba: ""Mkataba wa Cairo" umeangamizwa na Marekani na nchi tatu za Ulaya."

Sayyid Abbas Araqchi ameandika kwenye akaunti yake ya X kwamba: "Kama ambavyo jitihada za diplomasia zilivyohujumiwa na Israel na Marekani mwezi Juni, "Mkataba wa Cairo" pia umeangamizwa na Marekani na nchi tatu za Ulaya."

Mchakato wa kuchukiza na wa aibu uliotufikisha hapa ni kama ifuatavyo:

Tulipokuwa karibu na duru ya sita ya mazungumzo ya nyuklia na Marekani, ghafla utawala wa Israel na kisha Marekani ziliishambulia Iran. Wakati Iran iliposaini makubaliano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) huko Cairo yaliyosimamiwa na Misri ili kuendelea na ukaguzi; na licha ya kushambuliwa kwa mabomu vituo vya nyuklia vya Iran, nchi tatu za Ulaya, chini ya mashinikizo kutoka Marekani, zilichukua hatua ya kuwekwa vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya watu wetu. Iran ilipoanza kutarisha mazingira ya kuwawezesha wakaguzi wa IAEA kufika kwenye vituo vyake vya nyuklia, kwa kuanzia kwenye maeneo ambayo hayakushambuliwa katika mashambulizi ya Juni na Julai, Marekani na nchi tatu za Ulaya ziliungana kuilaani Jamhuri ya Kislamu katika Bodi ya Magavana ya IAEA. Sasa ni wazi kwa wote kwamba: Si Iran inayotaka kuibua mgogoro mpya. Hawaelewi nia zetu nzuri. Nchi tatu za Ulaya na Marekani zinataka kuibua mvutano, na zinajua vyema kwamba kusitishwa rasmi Makubaliano ya Cairo ni matokeo ya moja kwa moja ya uchochezi wao wenyewe.

Msisitizo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwamba Makubaliiano ya Cairo yameharibiwa na Marekani na nchi tatu za Ulaya zinazojulikana kama Troika ya Ulaya (Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza) unaonyesha ukweli mchungu kwamba lengo halisi la Magharibi katika mienendo yake ya hivi karibuni na Iran, kuanzia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran hadi kuhitimishwa kwa Makubaliano ya Cairo, halikuwa kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia za amani, bali hasa kutumia udanganyifu na kisha kuishinikiza Iran kutoa taarifa sahihi kuhusu kiwango cha uharibifu wa vituo vya nyuklia vya Iran kupitia wakaguzi kutoka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

"Makubaliano ya Cairo" yalifikiwa baada ya mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, kwa upatanishi wa Misri na ushirikiano wa Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki. Lengo kuu la makubaliano hayo lilikuwa kuendelea na ukaguzi na kujenga uaminifu wa pande zote ili njia ya mazungumzo ya nyuklia iweze kufunguliwa tena. Hata hivyo, Marekani na nchi tatu za Ulaya, kupitia mashinikizo ya kisiasa, vikwazo vipya na kutoaminiana katika mchakato wa utekelezaji wa makubaliano hayo, zimekwamisha kabisa utekelezaji wa "Makubaliano ya Cairo" na kuzuia kufikiwa kwa malengo yake.

Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Badr Abdelatty. Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, na Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran 

Hatua na mbinu kadhaa zimetumiwa na Marekani na Troika ya Ulaya ili kuharibu makubaliano hayo:

1. Shambulio la awali dhidi ya diplomasia: Kabla ya duru ya sita ya mazungumzo kuanza, Israel na kisha Marekani zilishambulia ardhi ya Iran. Kitendo hiki kilidhoofisha mazingira ya kidiplomasia na kusababisha hali ya kutoaminiana.

2. Msaada wa Ulaya: Baada ya kusainiwa makubaliano hayo huko Cairo, nchi tatu za Ulaya (Ujerumani, Ufaransa na Uingereza) zilifuata mbinu ya uharibifu ya Marekani, na badala ya kuunga mkono makubaliano hayo kivitendo, zilifanya jitihada za kufufua vikwazo vya Baraza la Usalama la UN dhidi ya Iran kwa kuhuisha utaratibu wa snapback.

3. Kupuuza utekelezaji wa makubaliano: Ingawa Iran ilianza kutayarisha mazingira ya kuwawezesha wakaguzi wa IAEA kufika kwenye taasisi zake za nyuklia; Marekani na Ulaya ziliharibu utekelezaji wa Mkataba wa Cairo kwa kuweka vikwazo.

4. Kujenga hali ya kutoaminiana: Ukaguzi ulitakiwa kuanza katika maeneo ambayo hayakushambuliwa kwa mabomu ya Marekani na Israel, lakini wakati huo huo, Marekani na Ulaya zimetumia propaganda chafu za kisiasa kuishutumu Iran kuwa haina uwazi katika miradi yake ya nyuklia. Mkanganyiko huu umedhoofisha makubaliano ya Cairo kutoka ndani.

5. Kufunga njia ya diplomasia: Hatimaye, kwa kuendeleza mashinikizo na vikwazo, Makubaliano ya Cairo hayakuwa na ufanisi wowote, na kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, "yameuawa," ikiwa na maana kwamba, haiwezekani tena kuendelea kuwepo na kutekelezwa.

Sasa nini matokeo ya hali hii?

- Kuongezeka hali ya kutoaminiana. Iran imegundua kwamba hata kwa ushirikiano na kusaini makubaliano, nchi za Magharibi hazizingatii ahadi na majukumu yao. Jambo hii limepunguza imani katika mazungumzo yajayo.

-Kuzidisha mvutano. Kushindwa Makubaliano ya Cairo kumeelekeza tena hali ya kikanda na kimataifa kwenye mzozo na mgogoro.

- Kudhoofisha jukumu la shirika hilo: Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, ambalo lilipaswa kuwa kitovu cha ujenzi wa uaminifu, lilipoteza uaminifu wake chini ya shinikizo la kisiasa kutoka Marekani na Ulaya.

-Fursa ya kidiplomasia iliyopotezwa na Magharibi: Mkataba wa Cairo ungeweza kufungua njia ya kupunguza mvutano na kurejea kwenye meza ya mazungumzo, hata hivyo kufeli mkataba huo kutokana na ukwamishaji wa Magharibi kumefunga njia ya diplomasia huku uwezekano wa kushuhudiwa mapigano zaidi ukiongezeka. 

Mwishoni tunapasa kusema kuwa Marekani na nchi tatu za Ulaya  zimesambaratisha Mkataba wa Cairo kwa kuibua mashinikizo ya kisiasa, vikwazo vipya, propaganda za vyombo vya habari na kupuuza utekelezaji wa makubaliano hayo. Mwenendo huu si tu umesambaratisha mkataba muhimu bali umeathiri pakubwa  hali ya kuaminiana, uthabiti wa kikanda na mustakabali wa mazungumzo ya nyuklia.