Tanzania yazionya BBC, CNN, DW na al-Jazeera ikisema vina nia ovu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133528-tanzania_yazionya_bbc_cnn_dw_na_al_jazeera_ikisema_vina_nia_ovu
Msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amevikosoa vyombo vya habari vya nje akivitaka kufuata maadili na misingi ya uandishi wa habari.
(last modified 2025-11-24T05:36:00+00:00 )
Nov 24, 2025 03:18 UTC
  • Tanzania yavikosoa vyombo vya habari vya nje ikivitaka kufuata maadili na misingi ya uandishi wa habari.
    Tanzania yavikosoa vyombo vya habari vya nje ikivitaka kufuata maadili na misingi ya uandishi wa habari.

Msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amevikosoa vyombo vya habari vya nje akivitaka kufuata maadili na misingi ya uandishi wa habari.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar Es Salaam, Msigwa amevitaja vyombo vya habari vya CNN, Aljazeera, BBC na DW akisema kwamba vimekuwa vikichapisha habari za upande mmoja zenye nia ovu kwa Tanzania. 

Sio haki kwa vyombo vya habari kuchapisha habari za upande mmoja na baadaye kusema kwamba maafisa wa serikali walipotafutwa hawakupatikana', alisema msigwa, akizitaka kuchapisha taarifa zinazozingatia 'usawa, haki na uwajibikaji.'

Msigwa hususan amekitaja chombo cha habari cha CNN kama kilichokiuka maadili kwa kuchapisha habari zilizojaa 'tuhuma' dhidi ya serikali bila kutoa nafasi kwa serikali kujibu.

Msigwa ametolea mfano makala ya hivi karibuni iliyotolewa na shirika la habari la Marekani CNN, makala ambayo imeibua mjadala mkali nchini humo.

Katika makala hiyo ambayo iliandaliwa na mwanahabari raia wa Kenya, Larry Madowo, ilitumia teknolojia za kisasa kubaini maeneo na umbali waliokuwa askari wakati wakiwafyatulia risasi waandamanaji kwenye miji ya Arusha na Dar es Salaam.

Kuhusu idadi ya watu waliouawa wakati wa maandamano ya Octoba 29, Msigwa amesema tathmini bado inaendelea na kwamba idara ya polisi ndio yenye mamlaka ya kutangaza ni watu wangapi walipoteza maisha, huku akisisitiza kuwa kazi moja wapo ya tume iliyoundwa hivi karibuni ni pamoja na hilo.

Kuhusu uvumi wa maandamano ya Desemba 9, Msigwa aliwaonya vijana wa Tanzania akiwataka kutojihusisha na vitendo vyovyote vya vurugu au kushawishiwa kufanya vurugu kwa lengo la kuharibu amani ya nchi.