Rais Macron wa Ufaransa atoa indhari: G20 inakaribia kusambaratika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133498-rais_macron_wa_ufaransa_atoa_indhari_g20_inakaribia_kusambaratika
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ameeleza katika hotuba isiyo ya kawaida aliyotoa katika mkutano wa nchi zinazounda G20 mjini Johannesburg, Afrika Kusini kwamba kundi hilo limepoteza uwezo wake wa kuwa na taathira ya kutatua migogoro ya kimataifa na kwamba linakaribia kusambaratika.
(last modified 2025-11-23T06:33:12+00:00 )
Nov 23, 2025 06:33 UTC
  • Rais Macron wa Ufaransa atoa indhari: G20 inakaribia kusambaratika

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ameeleza katika hotuba isiyo ya kawaida aliyotoa katika mkutano wa nchi zinazounda G20 mjini Johannesburg, Afrika Kusini kwamba kundi hilo limepoteza uwezo wake wa kuwa na taathira ya kutatua migogoro ya kimataifa na kwamba linakaribia kusambaratika.

Macron ametoa indhari hiyo na kubainisha kuwa, kundi hilo linapoteza uwezo wake wa kuwa na taathira na ushawishi katika utatuzi wa migogoro ya kimataifa, jambo ambalo linauweka uwepo wake hatarini.

Kwa mujibu wa rais wa Ufaransa, inazidi kuwa vigumu kwa wanachama wa kundi hilo kuwa na muelekeo wa pamoja katika uga wa masuala ya usalama kwa sababu hakuna umoja unaohitajika miongoni mwao. Macron amesema, anaamini kwamba G20 sasa "inakaribia kusambaratika".

"Yamkini G20 inakaribia mwisho wa mzunguko wake. Tuko katika mazingira ya kijiopolitiki ambapo ni vigumu sana kutatua migogoro mikubwa ya kimataifa katika meza hii, ikiwa ni pamoja na kuzingatia wanachama ambao hata hawapo hapa leo. Ni vigumu kwetu kufikia kiwango cha pamoja katika uga wa kijiopolitiki" ameeleza rais wa Ufaransa katika hotuba yake hiyo.

Wakati huohuo, viongozi wa G20 wameahidi katika tamko lao la pamoja walilotoa kwenye mkutano wa kilele kufanya kazi kwa ajili ya kuleta amani "ya haki, kamili na ya kudumu" nchini Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, na Ukraine.

"Tukiongozwa na Madhumuni na Kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwa ukamilifu, tutafanya kazi kwa ajili ya amani ya haki, kamaili, na ya kudumu nchini Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eneo la Palestina Linalokaliwa na Ukraine," limeeleza tamko la mwisho la mkutano huo lililotolewa jana Jumamosi mjini Johannesburg.../