Ulaya yazungumza na Zelensky kumshawishi asikubali mpango wa Trump
Duru za habari zimeripoti kuwa, Kansela wa Ujerumani, Rais wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Uingereza wamefanya mazungumzo ya simu na kujadiliana mpango mpya wa amani wa serikali ya Marekani katika kadhia ya Ukraine na kujaribu kumzuia Zelensky asiukubali mpango huo wa Trump.
Shirika la habari la Interfax limeripoti habari hiyo na kumnukuu msemaji wa serikali ya Ujerumani, Stefan Cornelius akisema kwamba, kansela wa nchi hiyo, Friedrich Mertz amefanya mazungumzo ya simu na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer na kujadiliana mpango wa amani uliopendekezwa na Marekani kuhusu suala la Ukraine.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, pande zote katika mazungumzo hayo pamoja na kukaribisha juhudi za Marekani za kukomesha mgogoro wa Ukraine lakini zimeonesha kuwa hazikubaliani na mpango wa hivi sasa wa Trump wa kutatua mgogoro huo. Stefan Cornelius ameongeza kuwa viongozi wa Ulaya wamekiri kwamba wakati wa kukomeshwa vita Ukraine umewadia na ni muhimu kutumia "mstari wa mbele wa vita" kama mahali pa kuanzia mazungumzo ili kufikia makubaliano ya amani.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Mertz, Macron na Starmer wameihakikishia Ukraine kwamba wataendelea kuiunga mkono kikamilifu na daima katika juhudi zake za kufikia amani ya muda mrefu na ya haki na wamekubaliana kuendelea kufuatilia na kulinda maslahi makuu ya Ulaya na Ukraine kwa muda mrefu.
Viongozi hao wa nchi za Ulaya pia wamekubaliana kwamba makubaliano yoyote yanayohusisha nchi za Ulaya, EU na NATO yatahitaji idhini ya washirika wa Ulaya, hivyo ni muhimu kwa washirika hao kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu suala la Ukraine.