Israel yaendeleza jinai Ukingo wa Magharibi, yaua Mpalestina mwengine
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i133478-israel_yaendeleza_jinai_ukingo_wa_magharibi_yaua_mpalestina_mwengine
Jeshi katili la utawala wa Kizayuni limeendeleza jinai na mashambulizi yake dhidi ya Wapalestina kwa kumuua shahidi Mpalestina mwingine na kuwateka nyara wengine wawili na kutokomea nao kusikojulikana. Jinai hiyo imefanyika kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2025-11-22T11:37:44+00:00 )
Nov 22, 2025 11:37 UTC
  • Israel yaendeleza jinai Ukingo wa Magharibi, yaua Mpalestina mwengine

Jeshi katili la utawala wa Kizayuni limeendeleza jinai na mashambulizi yake dhidi ya Wapalestina kwa kumuua shahidi Mpalestina mwingine na kuwateka nyara wengine wawili na kutokomea nao kusikojulikana. Jinai hiyo imefanyika kwenye Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Shirika rasmi la habari la Palestina WAFA, limethibitisha habari hiyo kwa kunukuu taarifa ya Wizara ya Afya ikisema kwamba, wanajeshi wa Israel wamevamia kijiji cha Tell cha magharibi mwa Nablus, Ijumaa jioni na wapiga risasi moja kwa moja wananchi wa Palestina kabla ya kuingia kwa nguvu ndani ya jengo walililoshambulia.

Naamani Ramadan, mkuu wa baraza la kijiji cha Tell amesema kuwa, wanajeshi wa Israel wamempiga risasi Younes Waleed Mohammad Shtayyeh mwenye umri wa miaka 24 na kumuua shahidi hapo hapo.

Mkuu huyo wa baraza la kijiji cha Tell ameongeza kuwa, vikosi vamizi vya Israel vilimwita baba yake Shtayyeh ambaye alithibitisha kuwa mwanawe ameuawa shahidi kabla ya wanajeshi wa Israel kuubeba mwili wake kwa gari la kijeshi na kuondoka nao. Baba wa kijana huyo wa Palestina amesema kuwa, Shtayyeh alikuwa mmoja wa maafisa wa polisi wa Palestina.

Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Palestina imesema katika taarifa yake kwamba vikosi vya Israel vimezuia timu za matibabu za jumuiya hiyo kumfikia kijana huyo na wakahakikisha kuwa hapewi msaada wowote wa dharura wa kimatibabu.

Chama cha Popular Front for the Liberation of Palestine kimeonya kwamba Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Wazayuni uko karibu kushuhudia Intifadha ya Tatu, kwani jinai na ukatili wa Israel unaongezeka kila siku na kuzidi kuchochea hasira za Wapalestina.