RSF: Tunafuatilia jitihada za kiimataifa za kurejesha amani Sudan
Kundi linalojulikana kwa jina la Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan (RSF) limesema kuwa, linafuatilia jitihada za kimataifa za kushinikiza kukomeshwa vita na mapigano angamizi nchini humo.
Katika taarifa yake hiyo, RSF imesema: "Vikosi vya Msaada wa Haraka vinafuatilia kwa shauku kubwa na vinathamini harakati kubwa za kimataifa za kurejesha amani nchini Sudan. Tunatangaza kwamba tunakubaliana kimalifu na kwa thati na jitihada hizo.
RSF imetoa tangazo hilo kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram katika hali ambayo rais wa Marekani Donald Trump amedai kwamba ameanzisha juhudi za kukomesha mgogoro wa Sudan kwa kushirikiana na nchi kama Saudi Arabia. Taarifa ya RSF imezishukuru pia nchi mbalimbali kama Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Misri -- kwa juhudi zao za upatanishi.
Mwezi Septemba mwaka huu, nchi hizo zilitoa taarifa ya pamoja zikitaka kuweko makubaliano ya miezi mitatu ya amani kwa ajili ya masuala ya kibinadamu nchini Sudan, yakifuatiwa na mchakato wa kisiasa wa mpito wa miezi tisa unaolenga kufikia makubaliano kamili ya amani na usalama wa kudumu nchini humo. Siku ya Jumatano, Baraza Kuu la Mpito la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattal Al Burhan chini ya jeshi la Sudan SAF nalo pia lilikaribisha jitihada hizo za kurejeshe amani Sudan.
Mgogoro uliosababishwa na uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF umewasababishia wananchi wa Sudan maafa makubwa. Mgogoro huo wa vita unaendelea tangu tarehe 15 Aprili 2023 na umeshaua maelfu ya watu na kuwafanya wakimbizi mamilioni ya wengine.